Na Joachim Mushi, Mbeya Vijijini
VITISHO na hofu ya vitendo vya ushirikina imebainika kuwa vikwanzo vya
mapambano ya baadhi ya watu wanaowatia mimba wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari katika Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini,
mkoani Mbeya.
Kauli hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na baadhi ya
wanakijiji kutoka katika baadhi ya vijiji vya Kata ya Tembela
walipofanya mahojiano kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi
alipotembelea vijiji hivyo.
Akizungumza mkazi wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Maria Kolneri alisema
baadhi ya wazazi hushindwa kuwawajibisha watu waliowatia mimba wanafunzi
kwa kuhofia usalama wao kwani familia iliyotuhumiwa hujenga uhasama na
familia ya mwanafunzi na hata kutoa vitisho.
Alisema katika kijiji hicho
ni vigumu kwa familia ya mwanafunzi aliyetiwa mimba kufuatilia ili
sheria ichukuwe mkondo kwani huwa kuna vitisho na vingine kutoka kwa
majirani wa familia hizo.
"Hapa ukianza tu kumfuatilia mtu aliyefanya kosa kama hilo unasikia
wanakijiji wanaanza kulalamika anataka kumfunga mwenzake sasa mtoto
atakaye zaliwa atalelewa na nani"? Watakusema huku familia yenye kosa
ikitoa vitisho hadi utaacha kufuatilia,"alisema.
"Ukitaka kupata kesi (uhasama) hapa kijijini kwetu mfunge kijana
aliyempa mimba mtoto wako", kila mwanakijiji anayekujua atakuona hufai
kwa madai kuwa umemwonea kijana uliyemshtaki," alisema mama huyo.
Aidha aliongeza kuwa baadhi ya familia uhofia vitendo vya ushirikina
(kulogwa) endapo utaendelea kufutilia kesi za mimba hivyo kukata tamaa,
jambo ambalo kwa sasa kijijini hapo limekuwa la kawaida.
Naye Nazareti Kibaga mkazi wa Kijiji cha Simambwe alisema kutokana na
hali hiyo wananchi wamekuwa wagumu kufuatilia kesi za mimba jambo ambalo
limefanya matukio hayo kuendelea licha ya changamoto zingine
zinazochangia uwepo wake.
"Hali hii imefanya mimba ziendelee na hakuna kesi yoyote dhidi ya
wanaowatia mimba wanafunzi", wazazi hawawajibiki, wananchi hawawajibiki
na viongozi nao hawawajibiki," alisema Kibaga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Willson
Mwamunyila alikiri uwepo wa matukio ya mimba kwa kiasi kikubwa kijijini
hapo lakini alisema kikwazo katika kushughulikia matukio ya mimba ni
uongozi kukosa ushirikiano kutoka kwa wazazi na mwanafunzi.
"Matatizo ya mimba yapo lakini wazazi na wanafunzi waliotiwa mimba
hugoma kutoa ushirikiano kwa viongozi ili wahusika washughulikiwe
kisheria.
Unakuta mtoto kapata mimba baada ya taarifa kukufikia unaenda
kwa mzazi wa mwanafunzi kuomba ushirikiano lakini wazazi wengine
wanakuzunguka wanazungumza na mwalimu kwenye shule husika na
wanamalizana wenyewe," alisema Willson Mwamunyila.
Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TGNP
