KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Hakimu wa Wilaya ya Karagwe,
mkoani Kagera, Peter Matete, ameacha kazi ghafla, huku akikwepa kutaja
sababu ya hatua hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kayanga, hakimu
huyo alisema kuwa ameamua kuacha kazi na tayari amemwandikia barua Jaji
Mkuu tangu Aprili 23 na kutoa saa 24 za kuacha kazi.
Matete alidai kuwa amesalimisha mshahara wake wa mwezi mmoja, huku
akisisitiza kutosema kile kilichomsukuma kuchukua hatua hiyo isiyokuwa
ya kawaida.
“Sitaki msumbuke kujua sababu zilizonifanya kuacha kazi. Sina
shinikizo lololote, mimi ni mtu mzima na nina akili timamu, mnalopaswa
kuelewa nimeacha kazi,” alisema Matete.
Wakati akichukua hatua hiyo, mahakama za Wilaya ya Karagwe katika
kipindi cha kuanzia Januari mwaka huu zimekuwa zikilalamikiwa na
wananchi, vyama vya siasa na asasi za kiraia kwa kuongezeka kwa vitendo
vya rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Katika kilele cha shutuma hizo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza, Februari 11,
mwaka huu aliitisha maandamano ya wachungaji 80 ya kupinga na kulaani
vitendo vya rushwa vinavyoendeshwa katika mahakama mbalimbali zilizopo
Wilaya ya Karagwe.
Alisema wananchi hasa wasiokuwa na kipato wamekuwa wakinyanyaswa
kwa kunyimwa dhamana na kutakiwa kutoa kiasi cha shilingi laki tano
ili kuweza kupewa dhamana, huku wengine wakipelekwa rumande bila hatia.
Hata hivyo kiongozi huyo wa kiroho alisema vyombo vya dini
vilikuwa vikichukiwa na mamlaka mbalimbali za juu kutokana na kusikika
vikilaani rushwa, ufisadi na wananchi kunyimwa haki zao za kikatiba.
NA
Mbeki Mbeki,Kagera
