Maandamano ya wafanyakazi. |
Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Dodoma limesema iwapo wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba wataongezwa posho, watafanya maandamano ya amani
nchi nzima.
Pia maandamano hayo yatatumika kuwasilisha madai ya wafanyakazi wanaoidai Serikali kutokana na malimbikizo ambayo wameshindwa kulipwa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa TUCTA wa Mkoa wa Dodoma, Dk Kamudu Ndenge, wakati akitoa tamko la viongozi wa vyama vya wafanyakazi Dodoma kwa vyombo vya habari kuhusu madai ya malipo wanayolipwa wabunge hao.
Alisema watashangaa ombi lao likikubaliwa na kuongezwa posho wakati kuna wahudumu wa idara mbalimbali ambako wafanyakazi wanapokea mishahara ya Sh 150,000 kwa mwezi.
"Rais (Jakaya Kikwete) asikubali kuongeza posho hiyo maana tumeshuhudia hadi muda huu Serikali ikishindwa kulipa madai ya wafanyakazi kwa maelezo ya kutokuwa na fedha," alisema.
Dk Ndenge alisema kimsingi hawapingi nia yao ya kulalamika na kutaka kuongezwa posho kutoka Sh 300,000 wanayolipwa sasa kwa sababu ni haki yao ya kikatiba zifike Sh 500,000 kiasi ambacho wanaamini kitawafaa katika kutatua matatizo yao ya msingi wakiwa Dodoma.
"Lakini tukiwa wote ni Watanzania tujiulize maswali, je kuna kiwango cha posho kinacholingana na Sh 300,000 kinacholipwa kwa watumishi wa Serikali wengi kwa mujibu wa nyaraka za Serikali wanaposafiri kikazi kuja hapa Dodoma ambako kuna maisha magumu?" Alihoji.
Aliendelea: “Ni kweli wakati wa Bunge viwango vya posho kwa watumishi wanaohudhuria vikao vya Bunge kutoka maeneo mbalimbali hubadilishwa na kulipwa Sh 300,000 au zaidi kwa sababu ya gharama kubwa za maisha?"
Alisema kama majibu ni hapana kwa maswali hayo kwa nini wajumbe wa Bunge la Katiba waone maisha ni magumu wakati kuna baadhi ya watu wanaoshiriki kikao hicho na wako katika ngazi za uamuzi lakini hawajathubutu kuwafikiria kuwaongezea posho.
Alisema kama viongozi wa wafanyakazi wa mkoa wa Dodoma kwa kutambua haki na usawa kwa kila binadamu na kwa watumishi wa umma wakiwamo wabunge hao, wanapinga nyongeza yoyote ya posho.
"Kitendo hicho kinadhalilisha wafanyakazi wengi wa nchi hii ambao viwango vya mishahara yao kwa mwezi havioani na gharama za maisha wanayoishi wakiwamo wafanyakazi wa Dodoma ambako wabunge wanapaona pagumu kuliko wengine," alisema.
Alisema ni muhimu wabunge waelewe kuwa wafanyakazi wamekuwa na madai ya kulipwa kima cha chini cha angalau Sh 300,000 kwa mwezi tangu mwaka 2006 hadi leo hakuna chombo chochote cha kisiasa kilichoona umuhimu wa madai hayo.
Alitoa mwito kwa Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicolous Mgaya kuandaa utaratibu utakaowezesha wafanyakazi wakiwamo wanataaluma kulipwa mishahara stahiki kulingana na taaluma zao, ili Taifa liondokane na tabia ya wataalamu kukimbia nchi kutafuta malisho mema katika mataifa mengine wakati wamesomeshwa na nchi hii.