Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewasili mjini London, Uingereza, kwa ziara rasmi ya siku tatu ya
kidola, moja ya ziara nadra sana kufanywa na viongozi wa nchi za nje
nchini Uingereza.
Rais
Kikwete na ujumbe wake aliondoka nchini usiku wa jana, Jumamosi, Machi
29, 2014, kuelekea London kwa ziara hiyo ya siku tatu ambako atakuwa
Mgeni Rasmi wa Serikali ya Uingereza.
Katika
ziara hiyo, Rais Kikwete ambaye ameambatana na Mama Salma Kikwete pia
anafuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Bernard Membe, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Mheshimiwa Hussein Mwinyi, Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Harrison George
Mwakyembe, Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Sospeter Muhongo,
Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Makuya na Waziri wa Biashara, Viwanda
na Masoko za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Nassoro
Mazrui.
Rais
pia anafutana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali (mst) J. Simbakalia na
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekolojia Mheshimiwa January
Makamba.
Baada
ya ziara ya Uingereza, Rais Kikwete atakwenda Brussels, Ubelgiji
kuhudhuria Mkutano wa Wanne wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na
Afrika – EU-Africa Summit – uliopangwa kufanyika kwa siku mbili –
Jumatano na Alhamisi, wiki ijayo kwenye Makao Makuu wa EU mjini
Brussels.
Mkutano
huo ambao mada yake kuu itakuwa ni Umuhimu wa Kuwekeza katika Watu,
Ustawi na Amani utahudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama wa EU na wale wa
Afrika akiwamo Rais Kikwete.
Mikutano
ya wakuu wan chi za EU na Afrika imefanyika mara tatu mpaka sasa
kuanzia na ule wa kwanza wa mwaka 2000 mjini Cairo, Misri ukifuatiwa na
ule wa Lisbon, Ureno mwaka 2007 na Tripoli, Libya mwaka 2010.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuhudhuria mkutano huo tokea ashike mamlaka ya kuongoza Tanzania mwishoni mwa 2005.
Rais Kikwete pia ameombwa kuhuduria mikutano mingine kadhaa ambayo itafanyika wakati wa Mkutano huo mkubwa.