WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameitaka Wizara ya Maji itafute njia
mbadala zitazosaidia kupunguza gharama za kuchimba visima ili wananchi
waweze kupata maji safi na salama.
“Wizara ya Maji angalieni uwezekano wa kupunguza gharama za uchimbaji
wa visima ili wananchi waweze kumudu kuchimba visima na wapate uhakika
wa maji safi na salama,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Machi 23, 2014), wakati
akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa yaliyofanyika kwenye
Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
“Hivi sasa nimeambiwa gharama ya kuchimba kisima mita moja ni sh.
150,000/. Je kama mtu anataka kuchimba kisima chenye urefu wa mita 180
au 200 itakuwaje? Ni dhahiri kuwa watu hawataweza kumudu hizo gharama.
Angalieni namna ya kuzipunguza,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa akifunga maadhimisho hayo kwa niaba ya
Rais Jakaya Kikwete aliwataka wakazi wa mkoa wa Dodoma waendelee
kuthamini dhana ya uchangiaji ili waweze kumudu kuendeleza miradi hiyo.
Aliwataka pia watunze vyanzo vya maji na kutunza miundombinu pamoja
na mitambo iliyonunuliwa kuendesha visima mbalimbali kwani maji yana
gharama. “Ninawasihi sana muitunze mitambo iliyowekwa kuendeshea visima
hivi kwani ni vifaa vya gharama sana,” aliongeza.
Mapema, Waziri Mkuu alizindua kisima cha maji kwenye kijiji cha
Mkonze nje kidogo ya mji wa Dodoma ambacho ujenzi wake umegharimu sh.
milioni 519.6/-. Kisima hicho chenye vichoteo 15, kitawanufaisha wakazi
5,887 kati ya 6,869 sawa na asilimia 85.7 ya wakazi wa kijiji hicho.
“Kabla ya kujengwa kisima hiki, ndoo ya maji ya lita 20 ilikuwa
ikiuzwa sh. 500/- lakini sasa ndoo moja inauzwa kwa sh. 100/- tu,”
alisema Mhandisi Mohammed Kali wakati akitoa taarifa ya mradi huo kwa
Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia aliweka jiwe la msingi kwenye tenki la maji katika
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo
4,500. Ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Novemba, 2014.
Akizungumza na wanajumuiya ya UDOM walioshiriki uzinduzi huo, Waziri
Mkuu alisema mradi huo mkubwa unaenda sambamba na ujenzi wa mradi
mwingine mkubwa wa maji taka (recycling plant). “Ninawasihi muangalie
uwezekano wa kutumia maji machafu yatakayosafishwa ili yatumike
kumwagilia miti na maua muweze kutunza mandhari ya UDOM,” alisema.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tenki hilo, Waziri wa Maji,
Prof. Jumanne Maghembe alisema hadi kukamilika kwake, mradi huo
utagharimu sh. bilioni 28. Alisema mradi huo unaojumuisha ujenzi wa
miundombinu ya maji safi na maji taka katika Chuo hicho, umefanyika
chini ya Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Maji nchini (WSDP).
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za
Tanzania, Burundi na Uganda, Bw. Phillippe Dongier alisema wao kama
wadau wa maendeleo, wanaona fahari kushirikiana na Wizara ya Maji katika
kuleta maendeleo ya sekta hiyo kwa Watanzania.
Uzinduzi wa miradi hiyo ya maji ni sehemu ya miradi 13 iliyopangwa
kuzinduliwa mkoani Dodoma kwenye maadhimisho ya maji ya mwaka huu. Hata
hivyo, mkoa huo una miradi 69 ya maji ambayo ujenzi wake unaendelea kwa
awamu tofauti.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, MACHI 23, 2014
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, MACHI 23, 2014