MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake Dk. Willibrod Slaa, wanatakiwa kushitakiwa kwa matukio ya umwagaji damu nchini, linachapisha hivyo gazeti la Uhuru katika taarifa ya Suleiman Jongo akiripoti kutoka Iringa.
Pia, vyombo vya dola vimelaumiwa kwa kukaa kimya bila kuwachukulia hatua
zakisheria licha ya kushiriki katika matukio yaliyopoteza maisha ya
Watanzania.
Hayo
yameelezwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba,
ambapo alisema licha ya viongozi hao kushiriki kwenye matukio mengi ya
vurugu na umwagaji damu, lakini bado wako nje wakiendelea kutanua.
Alisema iwapo uchunguzi wa kina utafanyika ni dhahiri Mbowe na Dk. Slaa
hawatasalimika na kwamba, ushahidi wa matukio upo hadharani.
Mwigulu alikuwa akizungumza katika Kijiji cha Magubike, kata ya Nzihi
wilayani Iringa wakati akimnadi mgombea wa CCM Godfrey Mgimwa, kwenye
uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga utakaofanyika Machi 16, mwaka huu.
Alisema Dk. Slaa na Mbowe wanahusika na vifo vya watu vilivyotokea
kwenye vurugu mbalimbali katika mikutano ya hadhara ya chama hicho.
"Hawa watu wameshiriki kwenye matukio mengi ya vurugu na yanafahamika, lakini hawajachukuliwa hatua. Uchunguzi wa kina ufanyike kwani wote hawa wanahusika moja kwa moja.
"Mikono yao imejaa damu za watu waliopoteza maisha Morogoro, Singida Arusha na maeneo mingine ya nchi yetu,"
alisema Mwigulu.
Alisema vurugu zote ambazo zimefanywa na CHADEMA lengo ni kufanikisha
mikakati yao kisiasa, jambo ambalo wananchi wa Kalenga wanapaswa
kuliepuka na kuwa makini nao.
Alisema kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka huu tayari vifo vya watu zaidi ya
nane vimetokea katika mikutano ya Chadema na kwamba, hali hiyo inapaswa
kuonywa vikali na wapenda amani wote.
Pia, alisema viongozi hao wamekuwa wakifadhili matukio ya vurugu kisha kijitokeza kusaidia familia za waathirika.
Akitoa mfano kwa Mussa Tesha, aliyemwagiwa tindikali mkoani Tabora
wakati wa uchaguzi mdogo jimbo la Igunga na Alphonce John, aliyetobolewa
macho wilayani Kahama, Mwigulu alisema viongozi hao walihusika na
mipango hiyo.
"Historia inaonyesha kuwa hawa watu wakiwa kwenye mikutano mauaji ni lazima. Tumechoka ni unyama huu sasa tunataka hatua kali zichukuliwe ili kulinda maisha ya watanzania,"
alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Kalenga kukataa viongozi hao
kwani, mara zote wamekuwa wakitumia ubabe na vitisho kutaka kupigiwa
kura.
"Ni vizuri wakamchagua kijana ambaye anaweza kufanya kazi katika mazingira ya amani na utulivu ili kuzitatua changamoto zilizopo,"
alisema Mwigulu.
Pamoja na hayo, alitumia nafasi hiyo kuweka wazi Watanzania wanatakiwa
makini na vyama vya siasa vyenye lengo la kuvuruga amani kuwa, CHADEMA
hunufaika na vurugu hizo kupitia wafadhili wao.