MGOGORO wa uongozi ndani ya Chadema, umeingia katika hatua nyingine baada ya makada wa chama hicho wanaopingana kimisimamo, kufunga ofisi za chama hicho mjini Mpanda kwa zaidi ya wiki sasa.
Makada
hao wamegawanyika na kuwa na kambi mbili tofauti, ambapo kila upande
umeweka kufuli lake na walinzi wake, kuhakikisha hakuna atakayevunja na
kuingia ofisini humo.
Ofisi
za chama hicho ambazo ziko katika Mtaa wa Mji wa Zamani mjini Mpanda,
kabla ya kufungwa zilikuwa zikitumiwa na viongozi wa chama hicho ngazi
ya wilaya na mkoa pamoja na viongozi Jimbo la Mpanda Mjini ambalo kwa
sasa Mbunge wake ni Said Arfi (Chadema).
Mvutano
huu wa uongozi uliibuka mwanzoni mwa wiki iliyopita, ambapo viongozi wa
chama hicho waliosimamishwa hivi karibuni, walifika ofisini hapo ili
waendelee na shughuli zao za kiofisi na kukuta ofisi zimefungwa kwa
kufuli lingine tofauti na waliloliweka wao.
Baada
ya kubaini hivyo, viongozi hao wa Jimbo la Mpanda Mjini, walilazimika
kuwahoji wenzao wa wilaya kulikoni ofisi za chama hicho kufungwa kwa
kufuli lingine, tofauti na hilo, ndipo walipojibiwa kuwa wao si viongozi
tena, kwa kuwa tayari wamesimamishwa uongozi.
Pia,
uongozi wa wilaya wa chama hicho, wanadaiwa kuwajibu wenzao hao kuwa
kwa kuwa wamesimamishwa uongozi, hawana mamlaka tena ya kufanya shughuli
zozote za chama ndani ya ofisi hizo.
Hivi
karibuni kikao cha maridhiano ya chama hicho kilichofanyika kwenye
ofisi cha chama hicho zilizopo katika mtaa wa Mji wa Zamani mjini hapa,
kiliwasimamisha uongozi baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho
mkoani hapa na wengine wawili kusimamishwa uanachama.
Kikao
hicho kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda Magharibi,
Masanja Katabi, kiliwasimamisha uongozi Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa
Katavi, John Malack, Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoani hapa, John
Matongo na Mwenyekiti wa Jimbo la Mpanda Mjini, Seif Sipia.
Wengine
ni Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini Joseph Mona, ambaye pia
ndiye Katibu wa Mbunge, Arfi na Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini,
Godfrey Kapufi.
Mbali
ya kusimamishwa uongozi, kikao hicho kimependekeza Kapufi na Diwani wa
Kata ya Makanyagio, Idd Nziguye wavuliwe uanachama, kama ilivyokuwa kwa
akina Dk Mkumbo na Mwigamba.
Pia,
kikao hicho pia kiliazimia Arfi achunguzwe, wakimtuhumu kudhamini
mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Maridadi mjini Mpanda,
unaodaiwa kutumika kuwakashifu Lema na Mnyika.
>>Habari leo
>>Habari leo