WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imebaini kuwepo mtandao wa wanaosafirisha wasichana wenye umri mdogo kutoka nchini na kuwapeleka China kisha kuwafanyisha vitendo vya ukahaba pasipo ridhaa yao.
Hayo
yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Wizara hiyo, Bernard
Membe, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala
mbalimbali yanayohusu wizara yake.
Alisema
mtandao huo ukishasafirisha wasichana hao na kuwafikisha China,
huwanyang'anya hati zao za kusafiria na kujikuta wakishindwa kurejea
nyumbani, hali inayowalazimisha kujikuta wakitumbukia kwenye biashara
hiyo.
Membe
alisema, taarifa ambazo wizara yake inazo ni kwamba, tayari mmoja wa
wasichana hao amefariki kwa kuuawa. Alisema mwezi uliopita walialikwa
kwenda nchini China, ambapo walibaini kuwepo kwa vitendo hivyo vya
kusafirisha wasichana kutoka Tanzania na kuwapeleka nchini humo ili
kuwafanyisha ukahaba.
"Inaelekea
kuna Watanzania wanaokwenda nchini China kwa kutumia nyaraka bandia,
huku wengine wakitumia paspoti ya nchi zingine wakati wao ni Watanzania
ili kusafiri nje ya nchi kwa lengo la kufanya biashara ambazo ni
haramu," alisema Membe.
Alisema
kutokana na kukithiri kwa hali hiyo, Rais Jakaya Kikwete, atakuwa na
ziara ya kutembelea nchi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ataenda
kujionea hali halisi ya kuwepo kwa vitendo hivyo.
Kwa
mujibu wa Waziri Membe, zaidi ya Watanzania milioni 3 wanaishi nje ya
nchi, lakini baadhi yao wapo wanaofanya ukabaha, biashara za dawa za
kulevya na ugaidi. "Kufanya vitendo hivyo ni kuivunjia heshima nchi
yetu," alisema na kuwataka Watanzania wasirubuniwe kwenda nje ya nchi
kwa kudhani kuwa maisha ya huko ni rahisi.
Aliwataka
wenye mitandao ya kuendesha madanguro ya ukahaba nje kwa kutumia
wasichana wa Kitanzania wajue kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Aliwataka Watanzania wanaoishi huko waishi kwa kufuata misingi ya nchi
na taratibu husika ili kulinda heshima ya nchi.
Wakat
i huo huo, Waziri Membe alisema wizara yake kwa kushirikiana na Mkuu wa
Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu, watatuma timu kwenda nchini
humo ili kutambua watu wanaoendesha biashara hiyo ili kuikomesha.
JWTZ kupelekwa Sudan Kusini
Katika
hatua nyingine, Waziri Membe, alisema Tanzania imekubali kupeleka
wanajeshi wake Sudan Kusini kwa ajili ya kushiriki wengine kulinda
amani. Alisema Tanzania imefikia hatua hiyo baada ya kuombwa kutokana na
kazi nzuri ambayo wanajeshi wa JWTZ wamefanya nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
"Kwa
sasa hivi maandalizi hayo yapo katika hatua za mwisho na Tanzania
itaendelea kuimarisha diplomasia ya ushirikiano baina ya nchi jirani
katika kulinda na kudumisha amani,"alisema Membe.
Mgogoro wa mpaka na Malawi
Kwa
upande wa mgogoro, alisema Juni, mwaka huu ujumbe wa Tanzania utakutana
na jopo la usuluhishi wa mgogoro huo kwa lengo la kujadili faida na
hasara za mpaka huo kuwa katikati ya Ziwa Nyasa.
Alisema mkutano huo ulikuwa ufanyike Mei, mwaka huu,lakini kutokana na Malawi kuwa na uchaguzi, mkutano huo umesogezwa mbele.
Uhusiano na Rwanda
Akizungumzia
uhusiano wa Tanzania na Rwanda, Waziri Membe, alisema kumekuwa na
msuguano sana baina ya nchi hizo, lakini Tanzania haina ugomvi na
majirani zake.