RAIS Jakaya Kikwete hajaongeza posho kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Sh 300,000 za sasa na kueleza kuwa hajawahi kupokea maombi ya nyongeza ya posho hiyo.
Badala yake amefanya marekebisho ya mpangilio wa posho hizo ambapo itabaki Sh 300,000 hiyo hiyo ya awali.
Maelezo
hayo ya Rais Kikwete yaliyotolewa kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano
wa Ikulu, Salva Rweyemamu yanabainisha kuwa maombi kutoka katika bunge
hilo aliyopokea ni kufanyia marekebisho mpangilio kwa posho hiyo na
amekubali na kuruhusu kufanya kama wajumbe walivyoomba.
“Kilichoombwa si nyongeza ya posho bali ni ile Sh 300,000 kupanga katika mpangilio tofauti na awali,” alisema.
Katika
mpangilio wa awali katika posho ya Sh 300,000 ilikuwa posho ya kujikimu
Sh 80,000 na Sh 220,000 posho maalum ya kuhudhuria vikao.
Katika
posho hiyo ya kuhudhuria vikao iligawanywa posho ya dereva kati ya Sh
40,000 na Sh 45,000 kwa siku, usafiri wa ndani yaani mafuta au teksi,
mawasiliano na matumizi mengine binafsi.Mchanganuo mpya haukutolewa na
Ikulu.
Mgawanyo
huo uliopitishwa na Rais uliwasilishwa kwake na Kamati ya Kushughulikia
Posho iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir
Kificho.
Kamati
hiyo ilikuwa na wajumbe sita nao ni William Lukuvi, Mohamed Abood
Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari.
Kamati
hiyo iliyoanza kazi Februari 19 iliongozwa na mambo manne likiwamo la
uhalisia wa gharama za maisha mjini Dodoma na aina ya wajumbe
walioteuliwa kwa kuainisha pato lao kabla ya kuwa wajumbe wa Bunge.
Pia
sheria kuhusu taratibu za posho, uwazi wa posho zinavyotolewa na
ulinganisho wa malipo ya kuzingatia aina za wajumbe. Kamati baada ya
kujiridhisha iliwasilisha mapendekezo yake kwenye mamlaka hiyo, ili
itafakari mapendekezo hayo na kutoa maelekezo.
Rweyemamu
alieleza msimamo huo wa Rais kuhusu posho kutokana na kauli iliyotolewa
juzi na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa
Dodoma kusema iwapo wajumbe hao wataongezwa posho na mamlaka za uteuzi
watafanya maandamano ya amani nchi nzima.
Aidha kumekuwapo na taarifa kuwa posho hiyo imeongezwa na kufika Sh 500,000.
“Mamlaka
ya uteuzi haiwezi kuongeza posho kutokana na kuwa haijawahi kupokea
maombi ya ongezeko la posho hiyo na wala haijaongeza posho hiyo kama
ilivyoelezwa katika baadhi ya vyombo vya habari,” alisema Rweyemamu.
Chimbuko
la hoja Februari 19 ikiwa ni siku ya pili ya kikao cha Bunge Maalumu,
Richard Ndassa Mbunge wa Sumve, ndiye aliibua suala hilo la posho
akisema Sh 300,000 kwa siku wanayolipwa wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba ni ndogo.
Pia
alidai wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameongezwa posho na SMZ jambo
ambalo linaleta tofauti bungeni lakini baadaye Katibu wa Baraza la
Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, alikiri wawakilishi walidai nyongeza
hiyo ya posho lakini SMZ haikuwajibu.
Wawakilishi
hao walidai wanapokuwa nje ya SMZ wanalipwa Sh 200,000 hivyo baada ya
kufika kwenye Bunge Maalumu na kubaini posho ya kujikimu ni Sh 80,000,
waliwasilisha maombi waongezwe kiasi kinachopungua, ambacho ni Sh
120,000 kwa siku.
Akiungwa
mkono na Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi, walihoji sababu za wao
kupewa posho hiyo wakati wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba
walilipwa Sh 500,000 walipokuwa wakikusanya maoni.
Kwa
mujibu wa wanaotaka nyongeza, mchanganuo wa matumizi yao ni kwamba
hadhi ya hoteli wanayopaswa kulala ni ya kuanzia Sh 70,000. Pia
wanahitaji mafuta ya gari, kulipa madereva na kutoa fedha kwa watu
mbalimbali wanaowaomba msaada.
Kutokana
na madai hayo ya wajumbe ya nyongeza ya posho kulizuka malalamiko
kutoka kwa watu mbalimbali wanaopinga nyongeza hiyo kwa madai iliyopo ni
kubwa na wengine wanasema inatosha.
Miongoni
mwa waliopinga hadharani nyongeza hiyo kutoka ndani ya bunge hilo ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto, Julius Mtatiro, Mbunge wa Karatu
Israel Natse, Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Nkasi
Mohamed Kessy.