Kampuni ya Strabag International GmbH inayotekeleza ujenzi wa barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kivukoni hapa jijini Dar es Salaam imetakiwa kuhakikisha kuwa inakamilisha ujenzi wa sehemu hiyo ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo kama mkataba wao unavyoelekeza.
Waziri wa Ujenzi Mhe.
Magufuli alitoa agizo hilo wakati akiwa katika ziara ya kukagua
maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara kwa ajili ya mabasi yaendayo
haraka jijini Dar es Salaam (Dar es Salaam Bus Rapid Transit – BRT)
ambao umeelezewa kuwa na changamoto nyingi kiasi cha kusababisha
usumbufu kwa watumia barabara hiyo kwa kipindi kirefu.
Akimpatia taarifa ya
utekelezaji wa mradi huo Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Patrick
Mfugale alimjulisha Waziri Magufuli kuwa kwa hivi sasa changamoto nyingi
zimefanyiwakazi na mradi unaendelea kusimamiwa kwa karibu ili
kuhakikisha kuwa hukuna ucheleweshaji zaidi katika hatua hii iliyobaki.
Mkataba wa ujenzi wa
barabara hizi pamoja na vituo vya mabasi ulisainiwa mwezi Desemba mwaka
2012 ukiwa umepangwa kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu kwa
gharama ya Shilingi bilioni 280.
Kwa upande mwingine Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Saddik ambaye aliambatana na
Waziri Magufuli katika ziara hiyo, amewataka wafanyabiashara
wanaoendesha shughuli zao ndani ya sehemu ambayo mkandarasi anaendelea
na kazi waondoke kwani hiyo mbali ya kuwa kinyime na taratibu za
uendeshaji biashara zilizowekwa lakini pia imekuwa ni moja ya kisingizio
kinachotolewa kwamba uendeshaji wa shughuli hizo unachangia kuchelewa
kukamilika kwa ujenzi huo.
Waziri Magufuli akizungumza
wakati wa kuhutimisha ziara hiyo, amemtaka mkandarasi kuhakikisha
anaukamilisha mradi huo kwa muda na viwango vilivyokusudiwa. “Na kwa
wale walio ndani ya eneo la ujenzi ni lazima sheria ichukue mkondo wake”
alisisitiza Waziri Magufuli huku akimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kindondoni Mhandisi Mussa Natty kuhakikisha anasimamia zoezi hilo la
kuondoa haraka wale wote wote walioingia katika eneo hilo la barabara
kinyume na sheria.
Aidha, Waziri Magufuli
alielezea kushangazwa kwake kwa kuchelewa kuondolewa kwa nyaya za
Tanesco katika maeneo ya City Squire na Morocco kwani fedha za
kutekeleza kazi hiyo tayari zimelipwa muda kirefu. “Ucheleweshaji wa
ainaa hii ndiyo unaotoa mwanya kwa mkandarasi kuanza kutoa visingizio
vya kutokamilika kazi hii kwa wakati” ametahadharisha Mhe. Magufuli.
Hata hivyo katika hatua
nyingine Mhe. Magufuli amemtaka mkandarasi kuharakisha taratibu za
kuifungua barabara hiyo upande wa kuingia Dar es Salaam ambako kwa sasa
hivi hakuna shughuli kubwa zinazofanyika ili kupungiuza adha ya
msongamano wa magari yanayopishana katika njia moja ya upande wa kutokea
mjini katika barabara hiyo ya Morogoro hasa kwa eneo kati ya Ubungo na
Kimara.