WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema askari 2,000
waliounda kikosi maalumu cha Operesheni Tokomeza Ujangili watalipwa
fedha zao kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya operesheni hiyo.
Nyalandu alitoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, kusema kuna
zaidi ya askari 2,000 waliounda kikosi maalumu kwa ajili ya operesheni
hiyo ya awamu ya kwanza hawakulipwa posho zao hadi sasa.
Akizungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali jijini Dar es Salaam jana
wakati wa kikao cha kujadili njia shirikishi za kutumia katika vita ya
ujangili, Nyalandu alisema watahakikisha wanalipa madeni yote ya askari
hao kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo huku akisisitiza kwamba zoezi
hilo ni endelevu na lilisitishwa ili kuondoa kasoro zilizojitokeza
wakati wa operesheni hiyo awamu ya kwanza.
“Hili ni zoezi endelevu, lilisitishwa kwa ajili ya kuibuka kwa
kasoro kadhaa… askari wote walioshiriki katika operesheni hiyo watalipwa
wakiwemo wale wa askari wanyamapori na wenzao wa Jeshi la Wananchi
(JWTZ), hatutaaanza awamu ya pili na madeni,” alisisitiza.
Kuhusu awamu ya pili ya operesheni hiyo itakayoanza muda wowote huku
jumuiya ya kimataifa ikiungana katika vita dhidi ya ujangili, ambapo
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) litaongoza
vita hiyo.
Kwa mujibu wa Nyalandu nchi mbalimbali zimekubali kuisaidia Tanzania
katika mikakati ya muda mrefu na mfupi ya kupambana na ujangili.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo ni Uingereza, Marekani, Ufaransa,
Ujerumani, Hispania, Japan na China huku akizitaja taasisi kubwa
zilizotia mkono kuwa ni Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika
(ADB) na Umoja wa Mataifa (UN).
Alisema nchi hizo zitasaidia kujua nchi ambazo soko la meno ya tembo
na faru lipo kwa ajili ya kuuzwa, ikiwemo askari wa kimataifa
(Interpol).
Nyalandu alisema kuna uhaba wa askari wa wanyamapori 3,767 na
kufafanua kuwa hivi sasa wapo askari 1,088 pekee na wanaohitajika ni
askari 4,855.
>>tanzaniadaima
