WANAFUNZI
wa chuo cha ualimu Kleruu kilichopo Gangilonga mjini Iringa, wamefanya
maandamano wakipinga kukosa huduma ya umeme kwa wiki ya tatu sasa baada ya
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwakatia.
Maandamano
hayo yaliyoanzia chuoni hapo jana kuelekea ofisini na hatimaye nyumbani kwa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, yalidhibitiwa na Jeshi la Polisi yakiwa yamekaribi
shule ya msingi Um-salam kwa kile kilichoelezwa kwamba hayakuwa na kibali..
Rais
wa serikali ya wanafunzi ya chuo hicho, Manfred Joachim alisema wametii amri ya
Polisi lakini watayafanya tena Jumatatu baada ya kukamilisha taratibu zote
ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha Polisi.
Joachim
alisema wameamua kutumia mbinu hiyo ili kuongeza msukomo kwa uongozi wa chuo na
serikali kuitatua kero hiyo.
“Hatuwezi
tena kujisomea usiku na mafunzo ya teknlojia ya habari na mawasiliani yaani ICT
yamesimama; wanafunzi wamekata tamaa, hawajui hatma yao wakati ada wamelipa,”
alisema.
Wakiwa
wamekusanyika katika uwanja wa michezo wa chuo hicho chini ya ulinzi wa Polisi,
kiongozi huyo alisema huduma ya maji nayo ni kero kubwa chuoni hapo.
“Wakati
mwingine zinaweza kupita zaidi ya siku mbili hatujaoga; yote hayo ni kwasababu
tuaambiwa na uongozi wa chuo kwamba hawana fedha za kulipia huduma hizo,”
alisema.
Makamu
Mkuu wa Chuo hicho, Anjelist Mlenga alisema uongozi wa chuo unawaonea huruma
wanafunzi hao lakini akakosoa taratibu wanazozitumia kudai huduma hizo.
Akiwa
hajui kiasi cha fedha kinachodaiwa kwa ajili ya huduma ya maji, Mlenga alisema
deni la umeme chuoni hapo ni zaidi ya Sh Milioni 2.5.
Alisema
Mkuu wa chuo hicho amekwenda wizarani kufuatilia fedha hizo kwakuwa wao ndio
wenye jukumu la kulipia huduma hizo.
“Mkuu
wa Chuo yupo wizarani, naomba muwe wavumilivu kwani hata kama atakubaliwa fedha
hizo, kwa taratibu za serikali inaweza kuchukua wiki nyingine kuzipata,”
alisema.
Akizungumzia
ombi la wanafunzi hao la kukifunga chuo hicho mpaka pale huduma hizo
zitakaporejea, Mlenga alisema “ ni jambo linalojadirika, tutaona mpaka wiki
ijayo hali itakavyokuwa na tutaangalia cha kufanya.”