JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kukanusha taarifa
za uvumi zinaosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo
vya habari kuwa kuna Watanzania wapatao 160 wamenyongwa nchini China kwa
kosa la kusafirisha madawa ya kulevya.
Wizara inapenda kuujulisha Umma kuwa hakuna Mtanzania yeyote aliyenyongwa kama inavyodaiwa kwenye mitandao na vyombo vya habari.
Aidha, taarifa hiyo ya uvumi imedai kuwa ndugu wa mmoja wa Watanzania hao ambaye kwa jina anajulikana kama Bw. Rajab Mohamed Ismail Mapusa wamekaa matanga kuomboleza kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Serikali ya China, Bw. Mapusa
yupo hai gerezani akitumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kuingiza
madawa ya kulevya nchini humo, na hivi karibuni alishiriki kuandaa
maonyesho ya utamaduni wa Kiafrika wakati wa kuadhimisha sherehe za
Mwaka Mpya wa China.
Wizara
inapenda kuwakumbusha Wanahabari kuandika taarifa ambazo ni sahihi
zisizopotosha Umma kwa kuzingatia weledi, maadili na ukweli kutoka
mamlaka zote husika.
Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
10 Februari, 2014
