Habari zinasema Maregezi alikutwa na mkasa huo
wilayani Bunda juzi saa 12:30 jioni, wakati akipiga picha tukio la
vijana wa chama hicho kumteka na kumpiga kijana anayedaiwa kuwa kada wa
Chadema.
Akisimulia mkasa huo akiwa katika wodi ya wanaume
Hospitali ya Bunda, Maregesi alidai kuwa alikabwa na viongozi wa chama
hicho wakati akipiga picha za tukio la kada huyo wa Chadema aliyeshushwa
kutoka ndani ya gari na kuanza kushambuliwa na vijana waliokuwa pamoja
na viongozi hao.
Alifafanua wakati akiendelea kupiga picha tukio
hilo, ghafla Mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa alimkaba kwa madai kuwa
atawaumbua na kusaidiana na kiongozi mwenzake ambaye alichukua kamera na
ghafla kundi la vijana wa chama hicho wakamvamia,kuanza kumpiga na
kumpora mkoba aliokuwa nao, kisha wakamfungia ndani ya chumba cha ofisi
yao.
“Ndani ya chumba nikaingizwa mimi na huyo kijana
anayedaiwa kada wa Chadema na kuanza kutupiga, ndipo mtu mmoja akasema
mtawaua hawa iteni polisi baadaye askari wa JKT walioletwa maalumu
wilayani Bunda kulinda Kata ya Nyansura ndiyo waliotufikisha Kituo cha
Polisi Bunda,” alibainisha Maregesi.
Alitaja vitu alivyoporwa kuwa ni kamera aina ya
Sony digital, risti zake, daftari la kuandikia habari (Note Book),
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, simu ya mkononi aina ya
Adio pamoja na vitu vingine mbalimbali.
Akizungumzia hali ya Maregesi mmoja wa madaktari
wa Hospitali ya Bunda, Dk Nimrod Mzuma alisema mwandishi huyo
anakabiliwa na maumivu makali katika uti wa mgongo, kichwani na mkono wa
kulia na kwamba alifikiswa hospitali hapo akiwa na watu wengine wawili
waliojeruhiwa katika tukio hilo pia.
Akizungumzia tukio hilo, Emanueli Imanani Katibu
wa Chadema wilaya anavitaka vyama vya siasa kuheshimu taaluma ya
uandishi wa habari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Fernandi
Mtui,alikanusha kuumizwa kwa Maregesi na kueleza kuwa ameonana na
mwandishi huyo kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi akiwa hana majeraha
yoyote.
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Mkoa
wa Mara (MRPC) Emanuel Bwimbo,alilaani tukio hilo akisema linavunja haki
ya upatikanaji habari na kwamba limefanywa na viongozi waliopaswa kuwa
mfano wa kuigwa.
“Tunaomba wamuombe radhi Maregesi na waandishi
wote, pia wamrudishie vifaa vyake haraka ili aendelee na majukumu yake.
Wasipotekeleza hayo chama kitachukua hatua ikiwa pamoja na kumsaidia
kuendesha kesi mahakamani ili kupata haki yake,”alisema Bwimbo.
CHANZO:MWANANCHI