Mkuu huyo wa wilaya ambaye ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa halmashauri ya wilaya ya Makete, wamesikitishwa na maafa hayo ambayo yameacha simanzi kubwa kwa wananchi hasa wamiliki wa nyumba hizo
Akizungumza na baadhi ya waathirika walioezuliwa nyumba zao Mh Matiro amewapa pole kwa janga hilo lililowakumba ambapo ameshuhudia mwenyewe hali ilivyokuwa ya baadhi ya nyumba kubomoka kuta zake, mapaa kusombwa pamoja na bati kupeperushwa mbali huku baadhi ya vipande vikionekana kunasa kwenye miti
Katika taarifa ya awali iliyotolewa kwa mkuu wa wilaya na Afisa Mtendaji wa kata ya Iwawa Bw. Festo Msigwa imesema kuwa jumla ya kaya nane zimepatwa na maafa hayo pamoja na jiko la shule ya msingi Ndulamo na kufanya jumla ya nyumba 11 kuathirika na janga hilo
Aidha mkuu wa wilaya ameagiza kijiji kufanya tahmini ya haraka ili ijulikane ni athari kiasi gani kimetokea akitolea mfano idadi ya bati na mali za wahanga hao kwa ujumla ili serikali ione namna ya kufanya haraka iwezekanavyo
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete ambaye naye alikuwepo eneo la tukio amesema kesho Jumatatu asubuhi na mapema atatuma timu ya wataalamu kufika kwa ajili ya kufanya tathmini ili ijulikane ni kiasi gani cha maafa na hasara iliyotokea
Afisa mtendaji wa kijiji cha Ndulamo Bw. Majuto Mbwilo amesema kwa sasa uongozi wa kijiji umewaombea wahanga kwnye nyumba za jirani ambapo ndipo wanapoishi hadi sasa wakati taratibu nyingine zikiendelea
Miongoni mwa wahanga ambaye nyumba yake mbali na kuezuliwa pia imebomoka yote bw.Imma Mahenge amesema wakati tukio hilo linatokea hakuwepo nyumbani hivyo anamshukuru Mungu kwa kumnusuru lakini anaumia kwa kuwa nyumba yake yote imesambaratika
Tukio hilo limetokea jioni ya jana Februari 15 majira ya saa 11 jioni