| NB-Picha haihusiani na tukio katika habari hii. |
Jeshi la polisi mkoani Mwanza linafanya
utafti wa kina kubaini askari mmoja wa kituo cha Nyakarilo wilayani
Sengerema anayetuhumiwa kuomba mchango wa fedha ya mafuta kwenye familia
ya mwanamke aliyefariki kwa kujinyonga.
Mwanamke huyo,Suzana James(28)mkazi wa
kijiji cha Nyanzenda wilayani hapa anadaiwa kuchukua uamuzi wa
kujinyonga kutokana kile kilichoelezwa na ndugu kwamba ni baada ya
kuugua ugonjwa wa kuchanganikiwa akili kwa muda mrefu.
Askari huyo akiwa na mgambo mmoja
alifika eneo la tukio hilo alhamisi iliyopita kufanya uchunguzi
kuhusiana na kifo cha mwanamke huyo aliyejinyonga kwa kutumia kitenge
alichokifunga juu ya mti wa mwembe umbali wa mita 200 kutoka nyumbani
kwake.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani
Mwanza,ambaye ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai,Joseph Konyo
akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa habari hizi alisema kitendo
hicho ni kinyume na utaratibu wa polisi.
''Tunafanya utafti kujua kilichotokea
hasa.Mimi kaimu RPC,ninayeshughulika na masuala ya uharifu najua mambo
mengi zaidi kwa hiyo,huyo askari akibainika kweli alichukua fedha hizo
atachukuliwa hatua za kisheria''alisema Konyo.
Aidha Konyo,alikiri kuwepo baadhi ya
askari ndani ya jeshi hilo ambao ni waovu wanaoweza kuchukua hela kwa
mazingira kama hayo kinyume na kanuni,taratibu na sheria za jeshi la
polisi nchini.
Pia alisema wapo watu ambao wamekuwa
wakitumia jina na wadhifa wake(RCO)kwa kujifanya polisi na kwenda kwenye
maduka ya wahindi yaliyopo jijini Mwanza kisha kuchukua kwa kusingia
wametumwa na RCO(Mkuu wa upelelezi mkoa).
Inadaiwa kabla ya kufika eneo la tukio
askari huyo alipiga simu kwa kaimu mtendaji wa kata ya Nyanzenda,Mathias
Wiliam akitoa maelekezo ya kumtaka mme wa marehemu,Simeon
Katisho(32)kuandaa mchango wa mafuta kiasi cha sh.100,000ya kuwarudisha.
Kwa
mujibu wa mme wa marehemu,Katisho baada ya kufanya uchunguzi huo kaimu
mtendaji wa kata ya Nyanzenda Mathias Wiliamu alimvuta pembeni na
kumuomba sh.100,000 zikiwa ni mchango wa mafuta ya askari hao.
Alisema kutokana na matatizo ya kufiwa
na mkewe hakuwa na kiasi hicho na hivyo kutoa sh.50,000 ambazo
alimkabidhi mtendaji huyo kisha kuwapatia askari na mgambo huyo ambao
waliongozana kutoka msibani hadi ofisi ya mtendaji wa kata.
Na Valence Robert- Mwanza