WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefanikiwa
kukusanya sh. bilioni 83.4 kufikia mwaka 2013/2014 ambazo zinatokana na
shughuli mbalimbali zilizofanywa na Idara ya Uhamiaji. Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh Pereira Ame Silima wakati wa
mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam akieleza mafanikio ya
Wizara.
Mh
Pereira alibainisha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2006/2007 zilikusanywa shilingi bilioni
14.2 ambapo kumekuwa na ongezeko la
bilioni 69.2 kufikia mwaka 2013/2014 ambayo ni moja ya mafanikio ya Serikali ya
awamu ya nne.
Mh
Pereira alibainisha kuwa Ongezeko hilo ni matokeo ya juhudi zilizofanywa na
Serikali katika kuboresha mifumo ya makusanyo ya maduhuli kwenye vyanzo
mbalimbali vya Wizara. Aliongeza
kuwa jumla ya magari 192 yalitolewa kwa idara hiyo, 93 yakiwa ni msaada ya
wafadhili.
Alitaja
vifaa vingine vilivyonunuliwa kwa ajili ya Idara hiyo ni pikipiki 206 na boti
mbili (02) ambazo hutumika kufanya misako na doria katika maeneo mbalimbali
nchini ikiwa ni hatua za maksudi katika kupambamna na uhalifu.
Kwa
upande wa jeshi la Polisi, Mh. Pereira alisema kuwa wamefanikiwa kupunguza
uhalifu kutoka makosa 53,268 mwaka 2005 hadi
kufikia 45470 mwaka 2013. Alitaja
sababu kubwa ya kupungua kwa vitendo vya uhalifu nchini kuwa ni ushirikiano
mzuri toka kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa ulinzi shirikishi,utii wa sheria
bila shuruti,vifaa vya kisasa kwa askari yakiwemo magari, pikipiki na boti kwa
ajili ya doria.
Wizara
ya Mambo ya Ndani ya nchi inaundwa na Jeshi la Polisi,Jeshi la Magereza,Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji,Idara ya Uhamiaji,Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa,Idara ya Huduma kwa Jamii.
