WALIMU KIGOMA WASITISHIWA KUKATWA MISHAHARA YAO

CWT

MGOGORO wa walimu wapatao 811 wa Halmashauri ya Ujiji mkoani KIGOMA, umemalizika baada ya Halmashauri hiyo kuridhia na kuacha mara moja kukata asilimia mbili za mishahara ya walimu hao kisha kupeleka fedha hizo kwenye Chama cha walimu Tanzania(CWT).
 
Taarifa ya walimu hao kwa vyombo vya habari, iliyosainiwa na Mwenyekiti wa walimu, K. Sabibi, imesema mgogoro huo ulidumu kwa miaka miwili na nusu na tangu Octoba ,2013, Halmashauri hiyo imekubali kusitisha makato hayo kwa waliokuwa wamejitosa kupigania haki zao.
 
‘’Shukrani kwa viongozi wote hasa mkuu wa wilaya ya Kigoma, Ramadhan Maneno na wasaidizi wake, waliohakikisha mgogoro huo unamalizika kwa amani’’ imesema taarifa hiyo.
 
Taarifa hiyo imemshukuru pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Eng.Boniface Nyambele kwa uelewa wake na kukubali kuchukua hatua za makusudi kwa kusimamisha makato hayo kwenda CWT yaliyokuwa yakifanyika kinyume cha sheria tangu mwaka 2011.
 
Wamesema makato hayo yalikuwa yakifanyika kinyume na sheria ya ajira na mahusiano kazini kama kifungu cha 61(4) na 5 kinavyoeleza.
 
‘’Tunapenda ifahamike kwa walimu wenzetu na umma wa Watanzania kuwa mgogoro uliokuwepo kati ya walimu wa Kigoma ujiji na mwajiri yaani Mkurugenzi, umekwisha malizika’’
 
‘’Kwa kuwa mgogoro huo umekuwa wa muda mrefu na vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa, tunavishukuru sana kwa kazi nzuri kwa kuhabarisha walimu wenzetu na wananchi’’ imesema taarifa hiyo.
 
Imeeleza kuwa, kuwepo kwa mgogoro huo kuliathiri utendaji kazi wa walimu hao kwa namna nyingi ingawa si kwa kiwango kikubwa.
 
Sanjari na hayo, walimu hao wamevikumbusha vyama vya wafanyakazi na waajiri, kufanya kazi kwa kufuata sheria za kazi siyo mazoea na kwamba ikumbukwe kuwa kukata mshahara wa mwajiriwa bila ridhaa yake ni kosa kama inavyofanya CWT kwa walimu kote nchini.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo