WAALIMU WENYE VIRUSI VYA UKIMWI MKOANI PWANI WALALAMIKIA WAALIMU WAO

BAADHI ya wanafunzi wa shule za msingi mkoani Pwani wenye virusi vya Ukimwi, wamesema baadhi ya walimu huwataka kimapenzi licha ya kuwaeleza ukweli juu ya hali zao kiafya.
 
Wametaka Serikali na asasi za kiraia kusaidia kushughulikia walimu na wanajamii wanaoshawishi watoto kwa ujumla kuingia kwenye uhusiano nao wa kimapenzi.
 
Wamesema changamoto hiyo, husababisha baadhi kupata tabu katika masomo yao hasa katika suala la ufaulu, kutokana na kujikuta wakipunjwa alama kwa makusudi wanapokataa kuingia uhusiano na walimu.
 
Hayo yalielezwa kwenye semina ya wiki mbili kwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 14 wanaoishi na VVU, iliyoshirikisha pia walezi na wazazi wao Kibaha mkoani Pwani.
 
“Mi sijaanza kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s), lakini najitambua kuwa naishi na virusi hivyo. Tatizo kubwa tunalokumbana nalo sisi watoto na hata wale ambao hawana virusi ni vishawishi vya ngono kwa watu wazima, kwa mfano mimi na rafiki yangu kuna walimu shuleni walitutongoza, ukikataa anakuchapa fimbo,” alisema mmoja wa watoto.
 
Baadhi ya watoto waliozungumza na mwandishi, walisema licha ya walimu, baadhi ya watoto wamejikuta katika wakati mgumu kutokana na kushawishiwa kimapenzi na jamaa bila kujali kuathirika kwao na virusi.
 
Walishukuru shirika linalotoa huduma za kichungaji kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi mkoani Pwani na Dar es Salaam chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam (Pasada) kwa msaada wa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya na kuishi kwa matumaini ili kutimiza ndoto zao kupitia mradi wa “Kivuko na Watoto”.
 
Mkuu wa Idara ya Elimu na Mafunzo wa Pasada, Nelson Chiziza alisema mradi wa Kivuko kwa Watoto unalenga kuboresha mahusiano na mawasiliano kati ya mzazi, mlezi na mtoto anayeishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kuwajenga kimaadili, kujua namna ya kuboresha afya zao na matumizi sahihi ya ARV’s.
 
Awali akifunga semina hiyo iliyoshirikisha watoto 22 na walezi wao, Mkurugenzi Mtendaji wa Pasada, Yohana Simon alisema mradi huo ulianza kwa majaribio mwaka jana baada ya mchakato wa uanzishwaji wake kuanza mwaka 2011 .

>>Habari leo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo