MABINGWA wa Mtani Jembe na washindi wa pili wa
michuano ya Mapinduzi, Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Jumamosi
watajitupa katika Uwanja wa Taifa, kuvaana na timu ya Mtibwa Sugar.
Mchezo huo wa kirafiki utakuwa wa mwisho kwa klabu ya Simba, kabla ya
kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, inayoanza kutimua vumbi Januari 25
mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Kocha msaidizi wa Simba,
Suleiman Matola, alisema wameamua kupata mechi moja katika uwanja wa
taifa kabla ya kuanza kwa ligi.
Matola alisema sababu kuu ya kuamua kucheza mchezo huo ni moja ya
sehemu yao ya kuipa timu yao mazoezi katika uwanja wa Taifa, ambao
itachezea mechi zake za nyumbani. Alisema wameamua kucheza mechi na timu
ya Mtibwa, kwa sababu wanaitambua bora wake, hivyo wakicheza nayo
inawapa maandalizi mazuri.
Matola alisema kuwa mchezo huo utafanyika majira ya saa 10 jioni,
ikiwa ni moja ya sehemu ya kocha wao Zdravko Lugarusic, kutaka timu
ngumu, ya kucheza na timu ya Simba.
“Haya ni maamuzi ya kocha mkuu Logarusic, anataka kuichezesha timu
yake na timu ngumu, ambayo itaipa mazoezi mazuri timu yake, kabla ya
kuanza kwaa ligi kuu,” alisema Matola.
Simba iliyorejea juzi jijini Dar es Salaam, ikirtokea Zanzibar katika
michuano ya Mapinduzi, ambapo ilifika hatua ya fainali na kupata
ushindi wa pili wa michuano hiyo.