mwanamme mmoja ameuawa kwa kupigwa na
mpini wa jembe na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Majaliwa
kutokana na kile kilichotajwa marehemu kudaiwa shilingi elfu 3 katika
kijiji cha Ibelansuha kata ya Ushetu tarafa ya Dakama wilayani Kahama
mkoani Shinyanga.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa mbili asubuhi katika kijiji hicho cha Ibelansuha.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP
Evarist Mangala amemtaja aliyeuawa kuwa ni bwana Magulu Mhangwa (35)
mkazi wa kijiji hicho ambaye aliuawa kwa kupigwa na mpini wa jembe
sehemu za ubavuni na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Majaliwa.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni kutokana na marehemu kumdai mtuhumiwa wa mauaji hayo kiasi cha shilingi elfu tatu alizokuwa anamdai.
Aidha kufuatia kudaiwa pesa hizo
mtuhumiwa alikasirika na kuamua kumpiga kwa mpini wa jembe na
kusababisha kifo chake papo hapo huku mtuhumiwa akifanikiwa kukimbia.
Kamanda Mangala amesema jeshi la polisi
linaendelea kufanya msako mkali wa kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa wa
mauaji huku akiwaomba wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa
kwa mtuhumiwa huyo.
