Mkuu wa Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, Lembris Kipuyo.
MKUU wa Wilaya (DC) ya Muleba, mkoani Kagera,
Lembris Kipuyo, amedaiwa kutumia vibaya mamlaka yake na kuwalazimisha
polisi kumkamata Diwani wa Kata ya Magatakalutanga, Geofrey Ezekiel
(CCM), kwa madai ya kumtishia maisha na kutaka kummwagia tindikali.
Habari kutoka Muleba zilisema kuwa Kipuyo amekuwa akitoa tuhuma
mbalimbali dhidi ya diwani huyo na kufikia hatua ya kumshitaki katika
vikao vya CCM vilivyoketi Januari 5 na 6 mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari hizo, diwani huyo alilazimika kuandika barua kwa uongozi wa wilaya wa CCM na kumshitaki mkuu huyo wa wilaya.
Kwa mujibu wa habari hizo, diwani huyo alilazimika kuandika barua kwa uongozi wa wilaya wa CCM na kumshitaki mkuu huyo wa wilaya.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa kutokana na hatua hiyo Kipuyo
alikimbilia polisi na kudai kuwa diwani amemtishia maisha na kutaka
kummwagia tindikali, jambo lililolilazimu Jeshi la Polisi kumkamata na
kumweka chini ya ulinzi.
“Hivi ninavyokwambia diwani huyo ameelekea nyumbani kwake na polisi
kwa ajili ya kwenda kufanya upekuzi,” alisema mtoa habari wetu.
Habari zaidi zinasema kuwa mgogoro huo unatokana na Kipuyo kuingia
katika vikao viwili vya CCM na cha Kamati ya Siasa ya wilaya,
akimtuhumu diwani huyo kuwa ni mla rushwa na amekuwa akitumia nafasi
yake ya uenyekiti kushirikiana na makandarasi kula fedha za miradi.
Chanzo hicho kilisema kuwa hata katika kikao cha Januari 6 cha Kamati
Kuu ya wilaya bado mkuu wa wilaya hiyo aliendelea kushusha tuhuma hizo
huku diwani huyo akiwa si miongoni mwa wajumbe waliohudhuria kikao.
“Hatua hiyo ndiyo ilimsababishia diwani huyo kulazimika kuandika
barua kwa uongozi wa wilaya kulalamikia kitendo hicho na Kipuyo
alivyobaini hilo akaamua kumbadilishia tuhuma na kufungua hiyo ya
kumwagiwa tindikali na kutishiwa maisha,” alisema.
Hata hivyo gazeti hili lililazimika kumtafuta Kipuyo ambaye alipigiwa
simu na kushindwa kupokea, badala yake alituma ujumbe mfupi wa simu ya
mkononi na kudai kuwa yupo kikaoni, huku akitaka kujua aliyempigia simu.
Akithibitisha kukamatwa kwa diwani huyo, mmoja wa askari wa jeshi
hilo (jina limehifadhiwa) kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo, alikiri
kukamatwa kwa diwani huyo na kuwa bado wanamshikilia kwa ajili ya
uchunguzi wa tukio hilo.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA
