KIJANA mwenye umri wa miaka 20 mkazi wa Kijiji cha Isagala, wilayani
Kishapu, mkoani Shinyanga, ameuawa na watu waliojichukulia sheria
mkononi wakimtuhumu kuiba kuku wanne.
Aidha katika tukio la wilayani Tarime mkoani Mara, mtuhumiwa wa
ujambazi wa kutumia silaha , Senso Mwita ameuawa katika kile
kilichoelezwa ni kwenye majibizano ya kurushiana risasi na polisi.
Kuhusu anayetuhumiwa kuiba kuku, Polisi imemtaja ni Ngaga Shija
ambaye alipewa kipigo na kisha mwili wake kuchomwa moto, alikuwa
akituhumiwa kuiba kuku hao katika kijiji cha Ikonda.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evaresti
Mangala, kabla ya kifo, Shija alikuwa nje kwa dhamana katika kesi
iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga, akikabiliwa na
mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kupatikana na mali ya
wizi.
Aliuawa juzi saa 2 asubuhi katika Kijiji cha Isagala Kata ya
Mwamashele wilayani Kishapu. Hata hivyo Kamanda alisema mmiliki wa kuku
wanaodaiwa kuibwa, hajafahamika.
Katika tukio la wilayani Tarime, mkoani Mara, mtuhumiwa wa ujambazi
wa kutumia silaha , inadaiwa alikuwa na wenzake wawili ambao
walijibizana na polisi kwa kurushiana risasi.
Mwita anayekadiriwa na umri wa miaka kati ya 25 na 30, inadaiwa
alikuwa akisakwa na Polisi muda mrefu kwa kuhusika na matukio ya
unyang’anyi wa kutumia silaha na mauaji katika Tarafa ya Ingwe.
Kamanda wa Polisi Tarime / Rorya, Justus Kamugisha alisema mwezi
uliopita kulikuwa na matukio ya mauaji ya watu katika vijiji vya
Keisangura , Nyamwaga , Genkuru, Mriba na Nyarero.
Alisema usiku wa kuamkia Januari 5, Polisi ilipata taarifa kutoka kwa
raia wema juu ya kuwepo na kuonekana kundi la majambazi katika
kitongoji cha Ntarechagini Kijiji cha Nyamwaga.
“Wakati askari wetu wakiwa njiani kuelekea katika kitongoji hicho,
ghafla walishambuliwa kwa kurushiwa risasi na majambazi watatu na hapo
ndipo askari wetu walianza kujibu mapigo na kufanikiwa kumjeruhi mmoja
wao kwa jina la Senso Magabe Mwita,” alisema Kamanda.
Kwa mujibu wa Kamanda, Mwita alikuwa na silaha aina ya SMG iliyofutwa
namba zake na risasi 21. Wenzake walitoroka na yeye alifariki kutokana
na majeraha ya risasi akiwa njiani kupelekwa hospitali ya wilaya.
Via habarileo
