WASHITAKIWA 10 wanaodaiwa kumwua
aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengodo Mvungi
wameiomba Mahakama iwatenganishe rumande kwa kuwa wanapigana na
kutishana kuuana.
Walidai hayo jana katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Sundi
Fimbo. Washitakiwa hao waliiomba Mahakama iingilie kati suala lao kwa
kuwa wakiwa rumande wamekuwa wanatishana kuwa watauana jambo ambalo ni
hatari.
Hata hivyo, Hakimu Fimbo aliamua
waendelee kukaa huko mahabusu na waelewane na kama jambo lolote
litatokea watapewa taarifa na Mkuu wa Gereza.
Washitakiwa hao walidai kuwa hawajuani
na wapo gereza moja, lakini wanatishiana kuuana na wameshapeleka
malalamiko yao kwa Mkuu wa Gereza lakini hajachukua hatua na kuiomba
Serikali ifanye uchunguzi ili ijue aliyefanya mauaji hayo.
“Serikali ikifanya uchunguzi haki
itatendeka kabla ya wao kuuana wakiwa mahabusu,” alidai mmoja wa
washitakiwa hao huku akionesha majeraha aliyopata mwenzake kutokana na
kupigana.
Wakili wa Serikali, Yasinta Peter,
alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe
nyingine ya kutajwa, Hakimu Fimbo aliamua kesi hiyo itajwe tena Desemba
19.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Chibago
Magozi (32) , John Mayunga (56), Juma Kangungu (29), aliyekuwa mlinzi wa
marehemu Dk Mvungi, Longishu Losingo (29), Masunga Makenza (40), Paulo
Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Zacharia Msese (33), Msungwa Matonya
(30) na Ahmad Kitabu (30).
Wanadaiwa kuwa Novemba 3 katika eneo la
Msakuzi Kiswegere, Kibamba Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam,
washitakiwa hao kwa pamoja walimwua Dk Mvungi kwa kukusudia.
chanzo: habarileo
