Okwi akilakiwa kwa shangwe na mashabiki waliofika kumpokea mapema leo jioni.
Okwi akiwa na baadhi ya viongozi wa timu ya Yanga waliofika uwanja wa ndege kumpokea mapema leo jioni,jijini dar
Okwi akionesha namba yake ya mashambulizi siku ya jumamosi
HATIMAYE mshambuliaji raia wa Uganda Emanuel Okwi ametua nchini leo majira ya saa tisa na nusu alasiri na kupokelewa na viongozi wa Yanga katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Okwi
ambaye amesajiliwa Yanga kwa miaka miwili na nusu kwa jumla ya dola
60,000 alitua nchini na ndege ya shirika la Rwanda mbali na viongozi
hao wa Yanga ambao ni Abdallah Binkleb, Musa Katabalo na Seif Ahmed
'Magari' pia alilakiwa na wanachama wachache ambao walijitokeza
uwanjani hapo kwa lengo la kushuhudia ujio wake.
Akizungumza
mara baada ya kutua uwanjani hapo Okwi ambaye amezaliwa Desemba 25,
mwaka 1992 alisajiliwa Simba akitokea SC Villa ya Uganda mwaka 2010
akiwa kinda wa miaka 17, akisajiliwa kwa dau la dola za Kimarekani
40,000 alisema "Mimi ni mchezaji na mpira ni kazi yangu, nimekuja
kuichezea Yanga na nitaitumikia kwa mapenzi yangu yote, nimekuja
kufanya kazi na si kuiangalia Simba, mkataba wangu na Simba
ulishaishaga.
Akizungumzia
mechi ya Yanga na Simba itakayofanyika Jumamosi ijayo alisema "Mimi
nipo fiti, nipo tayari kucheza mechi ya Simba, nimejiandaa kikamilifu,
ila mwenye maamuzi ya mwisho ya mimi kucheza au kutocheza ni kocha,
kama atanipanga nitafurahi zaidi."alisema Okwi ambaye amejiunga kambini
na wenzake jana jioni kwenye hotel ya Protea iliyopo Oyesterbay jijjini
Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya Nani Mtani Jembe
Jumamosi.
Kuhusu
utata wa usajili wake Yanga, Okwi alisema "Mimi hayo mambo siyajui,
nimeyaacha mikononi mwa viongozi wa Yanga ndio watakaomaliza hilo
suala."alisema Okwi ambaye baada ya mkataba wake na Simba kuisha
Desemba mwaka jana aliongezewa mkataba wa miaka miwili na Simba kabla
hajaanza kuutumikia akahamia Etoile du Sahel ya Tunisia ambako aliuzwa
kwa dola za Kimarekani 300,000 fedha ambazo Simba wanazisotea mpaka
leo kwa kile walichoeleza kuwa Etoile haijawalipa.
Kufuatia
hali hiyo, Simba walipeleka malalamiko yao Fifa kuishtaki Etoile ambayo
nayo ilipeleka malalamiko ya Okwi kuwa ametoroka kwenye klabu hiyo,
ambayo hata hivyo alidai alikalishwa benchi miezi mitatu bila
kuchezeshwa wala kulipwa mshahara wake kitu ambacho kilimfanya atimkia
nchini kwao Uganda miezi michache iliyopita na Shirikisho la Soka la
Uganda (FUFA), lilimuombea kibali mchezaji huyo Fifa ili ajiunge na
klabu ya Sports Clab Villa ili kulinda kiwango chake na Fifa
ilimuidhinisha kuichezea klabu hiyo kwa muda wa miezi sita suala lake likiwa linashugulikiwa na tayari ameichezea klabu hiyo kwa miezi miwili.
Tayari
Fufa wameiandikia Fifa barua kutaka ufafanuzi wa usajili wa mchezaji
huyo Yanga kwa vile alizuiwa kucheza michuano ya kufuzu kucheza fainali
za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kwa vile hajamaliza
matatizo yake na Etoile du Sahel.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb alisema
"Baada ya mechi ya Jumamosi tutatoa ufafanuzi zaizi kuhusu usajili wa
Okwi, sisi hatujakurupuka, tumemsajili kwa ajili aweze kutusaidia
kwenye mechi zetu za kimataifa, tunaenda kupeperusha bendera ya
Tanzania hivyo Simba wawe wazalendo, kumsajili Okwi ni kama kunogesha
'ice' kwenye keki, tunalenga kuhakikisha michuano ya klabu bingwa
mwakani tunafika mbali.
Kauli
ya Binkleb imekuja kukiwa kwa mahasimu wao Simba kunawaka moto kwa
wanachama kumshinikiza mwenyekiti wao Ismail Aden Rage kujiuzulu huku
wakimtuhumu kutafuna dola laki tatu za mauzo ya Okwi kitu ambacho Rage
anakipinga vikali kwa kusema hajatafuna fedha hizo na kuweka ngumu
kujiuzulu.