JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIAWIZARA YA MALIASILI NA UTALI
TAARIFA KWA UMMA
Gazeti la kila wiki la Dira ya Mtanzania toleo la, Jumatatu, 18 Novemba, mwaka 2013, limechapisha habari yenye kichwa cha habari, “Siri nzito ya Kagasheki yagundulika na Mwandishi Sophia Yamola”.
Katika habari hiyo, Gazeti hili linadai kuwa Balozi Kagasheki ambaye ni Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii anaudanganya umma katika wimbi la kamatakamata ya Shehena ya Meno ya Tembo na kuwa ni usanii mtupu kwani ametengeneza mchezo wa sinema na kuonesha meno ya zamani lengo ili aonekane anakamata.
Aidha, Gazeti hili linadai kuwa taarifa za makala hayo zimetolewa na mtumishi wa wizara ambaye anafahamu udhaifu wote katika idara ya wanyamapori na kudai kuwa haina uwezo wa watumishi, bajeti na vitendea kazi. Katika makala hiyo zimetolewa takwimu kuimarisha hoja hiyo. Tunapenda kuufahamisha kuwa habari hizo si za kweli. Ni uongo unaolenga kuupotosha umma na kubeza juhudi za Serikali katika vita dhidi ya ujangili na kuichafua wizara kwa umma ili zoezi zima la kupambana na ujangili lionekane halina maana na analiita kuwa ni usanii mtupu.
Mheshimiwa Waziri Balozi Kagasheki (Mb) na Wizara kwa ujumla yuko makini na kazi yake na hafanyi dhihaka wala utani katika masuala mazito ya kitaifa. Aidha Vita dhidi ya ujangili ni vita halisi na inaendeshwa na Serikali kwa kutumia vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Ni zoezi makini, lina Baraka zote za Rais na Amiri Jeshi Mkuu na si kazi ya mtu mmoja au Waziri peke yake.
Tunapenda kufahamisha umma kuwa zoezi hili ni ghali na linaendeshwa kwa kutumia pesa za walipa kodi kwa manufaa ya Taifa. Wizara hii imepewa dhamana ya kulinda na kuhifadhi wanyamapori kwa niaba ya watanzania na ulimwengu kwa ujumla kwa faida ya Kizazi cha sasa na kwa vizazi vijavyo. Hili ni jukumu kubwa na Wizara ipo makini kutekeleza jukumu hilo. Kazi inayoendelea ya kutokomeza ujangili ni nzito, ni dhahiri, ni nyeti na Juhudi hizi hazipashwi kubezwa. Kwa Mhariri makini na Mzalendo hakupashwa kuandika Makala dhaifu isiyozingatia taaluma kwa kutoa takwimu ambazo hazina ukweli wala mashiko.
Wizara inaomba wananchi kuipuuza makala hiyo na waendelee kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za kuwezesha kubaini na kukamata majangili na hatimaye kutokomeza mtandao wa ujangili.
C.K. Rumisha
Msemaji wa Wizara
19/11/2013