Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Bi Olive Mugenda.
WANAFUNZI 19 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, wametimuliwa chuoni na kutozwa faini kwa kuhusika kwenye maandamano yaliyotokea baada ya kupatikana kwa vifaa vya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka chuoni humo.
Vifaa hivyo vilipatikana na
wanafunzi vikiwa vimefungiwa katika kituo cha biashara cha chuo hicho
jioni ya Machi 15, ambapo pia palikuwepo maafisa kadha wa IEBC.
Barua nne zilizotumwa kwa wanafunzi
hao kuwafahamisha kuhusu hatua zilizochukuliwa zilisema wamefukuzwa kwa
mihula miwili, na watahitajika kulipa faini ya Sh30,000 kila mmoja
watakaporudi chuoni.
Barua hizo zilizoonekana na Taifa Leo, zilitumwa kwa Mabw Odhiambo Justus Onyango, Omondi Jilali Ochieng, Olweny Steve Rundu na Mathai George Kamau.
“Imeamuliwa kuwa ufukuzwe kwa
kipindi cha mihula miwili ili urudi chuoni katika muhula wa kwanza wa
mwaka wa 2014/2015. Utahitajika pia kulipa Sh30,000 kugharamia uharibifu
uliotokea,” sehemu ya barua hizo ilisema.
Ilisemekana wanafunzi hao walifika mbele ya kamati ya nidhamu Agosti 8, mbali na uchunguzi kufanywa kubainisha ikiwa walihusika.
Uchochezi
Baadhi ya makosa waliyopatikana nayo
ni kusababisha ghasia chuoni, kupatikana na vifaa vya IEBC, kuchochea
wanafunzi, kuendeleza shughuli za wageni chuoni bila ruhusa na
kuzungumzia wanahabari chuoni bila idhini inayostahili.
Tukio hilo lilishuhudiwa wakati
kulikuwepo utata kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais, ambapo muungano wa
Cord ulikuwa umepinga matokeo ya kutangazwa kwa Uhuru Kenyatta kama
mshindi.
Baada ya tukio hilo, IEBC ilitoa
taarifa kupinga madai kuwa vifaa hivyo vilikuwa vinatumiwa kubadilisha
matokeo ya uchaguzi, na kusisitiza vilitumika katika kura ya mwigo na
vilihifadhiwa hapo vikisubiri kupelekwa katika bohari lao.
IEBC pia ililaumu baadhi ya
wanasiasa kuchochea wanafunzi hao. Kati ya wanasiasa waliowasili mahali
hapo siku hiyo walikuwa Mbunge wa Budalangi Ababu Namwamba, na Millie
Odhiambo wa Mbita.