WANAUME watatu waliokamatwa mtaani Kawangware Jumapili
iliyopita walipodaiwa kulewa baada ya kuvunja benki, Jumatatu
walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya wizi.
Bw Cleophas Musembi, Bw Robert
Gikenyi Nyang’au na Bw Charles Kimaiywa walishtakiwa kwa kuvunja tawi la
Kawangware la benki ya Barclays, na kuiba takriban Sh330,000 na mtambo
wa DVD wa benki hiyo.
Ilidaiwa washukiwa walishirikiana na
watu wengine ambao hawakuwa mahakamani kutenda kosa hilo usiku wa
Agosti 31 na Septemba 1 mwaka huu.
Bw Musembi na Bw Gikenyi walikabiliwa na shtaka la ziada la kupatikana na mali iliyoshukiwa kuwa ya wizi.
Kulingana na shtaka wawili hao
walipatikana na mtambo wa DVD ulioibwa kutoka tawi la Kawangware la
benki ya Barclays, na Sh2,900 zilizoshukiwa kuwa sehemu ya zilizoporwa
wakati wa kisa hicho.
Mahakama iliambiwa kwamba
walipatikana na mtambo huo na pesa hizo nje ya benki hiyo muda mfupi
baada ya majambazi kuvunja na kupora mali usiku wa Agosti 31.
Kila mshukiwa alikanusha mashtaka lakini polisi wakaomba wasiachiliwe kwa dhamana kwa sababu uchunguzi haujakamilika.
Kiongozi wa mashtaka Inspekta Justus Mugambi Imaana aliambia mahakama kwamba polisi walitaka kuwahoji washukiwa kwa siku tatu.
Rumande
Hakimu Mwandamizi wa Kibera Bi
Letizia Wachira alikubali ombi lake na kuagiza wazuiliwe katika kituo
cha polisi cha Kabete hadi Septemba 4 watakaporudishwa mahakamani.
Mnamo Jumapili, polisi walisema
waliwakamata washukiwa watatu waliolewa wakisubiri wenzao kwenye gari
nje ya benki ya Barclays mtaani Kawangware wakati wa kisa cha wizi.
Walisema baadhi ya washukiwa
waliokuwa ndani ya benki wakitekeleza wizi walifanikiwa kutoroka na
kwamba walipata vyombo walivyotumia kuvunja na kuingia katika benki
hiyo.
