MWENYE kampuni ya mabasi ya City to City iliyohusika kwenye ajali katika eneo la Ntulele, Narok, ambapo watu 41 waliuawa Alhamisi iliyopita amekamatwa.
Afisa mkuu wa
polisi Narok, Bw Peterson Maelo alithibitisha Jumapili kwamba
mfanyabiashara huyo ambaye alijitokeza katika baadhi ya vyombo vya
habari wiki jana kutetea kampuni hiyo amekamatwa.
Bw Maelo
alisema mfanyabiashara huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha
Muthaiga, Nairobi, na atafikishwa mahakamani Jumatatu.
“Nathibitisha
kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo amezuiliwa katika kituo cha
polisi cha Muthaiga na atafikishwa mahakamani kesho asubuhi,” akasema Bw
Maelo.
“Tutashtaki
kampuni kwa makosa ya kukiuka sheria za trafiki na walionusurika
wameandikisha taarifa kuhusu yaliyotendeka,” akasema Bw Maelo.
Lakini
alipokuwa akisema hayo, polisi hawakuwa wamemkamata dereva wa basi hilo.
Bw Maelo alisema polisi wanafuatilia habari kwamba mshukiwa amelazwa
katika hospitali moja ya kibinafsi mjini Kisii na inashukiwa analindwa
na watu wakuu serikalini.
“Tunafuatilia
habari ambazo bado hatujathibitisha kuhusu dereva wa basi hilo na
anayemlinda ili asichukuliwe hatua za kisheria. Tumewasiliana na wenzetu
wa Kaunti ya Kisii ili wachunguze madai hayo,” akasema Bw Maelo.
“Nilimuona
akishuka kutoka basi hilo. Jamaa zake waliniambia amelazwa katika
hospitali moja mjini Kisii,” akasema manusura mmoja aliyeomba tusitaje
jina lake.
Wakati huo huo, mili tisa ya waathiriwa wa ajali hiyo ingali katika mochari ya hospitali ya Wilaya ya Narok Kaskazini.
Mkurugenzi wa
Afya, Dkt Wago Dulacha, alisema mili 32 tayari imechukuliwa na
kusafirishwa hadi Homa Bay kwa mazishi na mingine imepelekwa hospitali
tofauti ambapo imehifadhiwa.
Dkt Dulacha
alisema kati ya mili tisa ni mmoja pekee uliotambuliwa na wamefanikiwa
kutambua jinsi waathiriwa 38 walivyokufa baada ya serikali ya Kaunti ya
Narok kulipa ada ya Sh5,000 iliyohitajika.
Akizungumza
na wanahabari nje ya hospitali hiyo, Dkt Dulacha alisema manusura
watano, akiwemo mtoto mmoja na wanawake wanne bado wamelazwa
hospitalini.
“Bado wanatibiwa kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani. Wengi wao wana majeraha mabaya,” akaongeza.
Manusura
Alisema wote waliojeruhiwa wako katika hali thabiti na wataruhusiwa kwenda nyumbani hivi karibuni.
Alisema
kufuatia ajali hiyo ya Alhamisi, manusura 32 walihamishwa hadi Hospitali
Kuu ya Kenyatta, Nairobi, ambako mmoja alifariki na kuongezea idadi ya
waliofariki kufikia 42.
“Waliohamishwa
hadi Kenyatta walikuwa na majeraha ya kichwa na wanahitaji uchunguzi
maalumu na hospitali hii haina vifaa vinavyohitajika,” akasema Dkt
Dulacha.
Millie
Akinyi, 20, ambaye alikuwa abiria katika gari hilo, alisema ni muujiza
kwamba yeye na mtoto wake mwenye miaka miwili walinusurika wakati wa
ajali hiyo. Bi Akinyi alipata majeraha madogo huku bintiye akikwaruzwa
usoni.
Na JOYCE BOKE Na GEORGE SAYAGIE