KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI AFUNGA MAFUNZO MAALUM YA KUTULIZA GHASIA MAGEREZANI, JIJINI DAR ES SALAAM

 Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(kulia) akikagua Gwaride Maalum lililoandaliwa na Wahitimu wa Kozi Na.09 ya Mafunzo Maalum ya kutuliza Ghasia Magereza leo Septemba 05, 2013 katika Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani kilichopo Ukonga, Jijini Dar es Salaam
 Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(kulia) akikagua Gwaride Maalum lililoandaliwa na Wahitimu wa Kozi Na.09 ya Mafunzo Maalum ya kutuliza Ghasia Magereza leo Septemba 05, 2013 katika Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani kilichopo Ukonga, Jijini Dar es Salaam


 Diana Marcus ambaye ni Askari wa Kike pekee aliyehitimu Mafunzo Maalum ya kutuliza Ghasia Magerezani akiwa amemkatamata Askari wa Kiume katika Onesho Maalum la kukabiliana na Wahalifu Magerezani wanapoleta fujo walilolionyesha mbele ya Mgeni Rasmi, Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini John Casmir Minja(hayupo pichani) leo wakati wa Ufungaji wa Mafunzo hayo ya Kutuliza Ghasia Magerezani
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja akitoa hotuba yake katika Ufungaji wa Mafunzo Maalum ya kutuliza Ghasia Magerezani leo Septemba 05, 2013 yaliyofanyika Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani.Picha na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza
--
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amewaasa Askari wa Jeshi la Magereza nchini  kuzingatia maadili ya kazi pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kujituma wakati wote wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kamanda Jenerali Minja ameyasema hayo leo wakati wa Ufungaji wa Mafunzo Maalum ya Kutuliza Ghasia Magerezani ya Kozi No.09 ya mwaka 2013 yaliyofanyika katika Kikosi Maalum cha kutuliza Ghasia Magerezani, Kilichopo Ukonga Jijini Dar es Salaam.


"Zingatieni maadili ya kazi pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwani ndiyo chachu ya mafanikio yoyote yale ya kazini au mafanikio yenu binafsi". Alisisitiza Kamanda Minja.


Aidha, akijibu hoja za changamoto mbalimbali zilizowasilishwa katika risala ya Wahitimu wa Mafunzo hayo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja alisema kuwa tayari Ofisi yake imeanza  kuchukua hatua ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo za upungufu wa vitendea kazi, makazi duni na upungufu wa Vyombo vya Usafiri kadri hali ya kifedha inavyoruhusu.


"Niwahakikishie kuwa kila jitihada zimekuwa zikifanyika na zitaendelea kufanyika kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi hatua kwa hatua matatizo haya kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu". Alisema Kamanda Minja.


Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Rajabu Nyange amesema kuwa Mafunzo hayo Maalum ya Kutuliza Ghasia Magerezani yamechukua muda wa takribani miezi minane(08) na yalifunguliwa rasmi tangu Januari 04, 2013 ambapo Wahitimu hao wamejifunza mbinu za Medani za kivita, Magwaride ya aina mbalimbali, kutuliza Ghasia Magerezani, Upekuzi Maalum, Escort za aina mbalimbali.


Vile vile Wahitimu hao wamejifunza Haki za Binadamu, Sheria na Ustawi wa Jamii, Ukakamavu na Ujasiri, Utafutaji wa Wafungwa waliotorokea kwenye misitu minene, Utafutaji wa Mifugo pamoja na Matumizi ya Vifaa vya kuzuia moto.


Jumla ya Wahitimu 51 wa Kozi hiyo Maalum ya Kutuliza Ghasia Magerezani wamehitimu Mafunzo hayo ambapo kati yao Askari wa Kiume ni 50 na Askari wa kike 1 ambapo walijiunga na Mafunzo hayo mara tu  baada ya kumaliza Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza Kozi Na.26 Chuo Kiwira, Mbeya mwaka 2012.


  Na
 Inspekta Lucas Mboje 
Jeshi la Magereza, 
Dar es Salaam


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo