WANAFUNZI SABA WAKAMATWA KWA KUPANGA NJAMA ZA KUCHOMA SHULE

WANAFUNZI saba wa kiume katika Kaunti ya Kirinyaga Kenya walitiwa nguvuni usiku wa kuamkia leo wakishukiwa kupanga njama ya kuchoma shule yao.
Wanafunzi hao kutoka shule ya upili ya Kagio walipatikana na lita tano za petroli na ambayo ilikuwa itumike kutekeleza uhalifu huo.

Walionaswa ni wanafunzi wa kidato cha nne na ambao wako kati ya miaka 17 na 18.

Kwa mujibu wa afisa mkuu wa polisi wa eneo hilo Bw Paul Odende, maafisa hao walifahamishwa na baadhi ya wanafunzi waliokeketwa na njama hiyo.

“Tulipata habari kuwa kuna baadhi ya wanafunzi waliokuwa na nia ya kuchoma shule yao. Ndipo tuliingia mahali hapo na kwa uhakika tukanasa washukiwa hao,” akasema.

Bw Odende alisema kuwa bada ya kuwahoji washukiwa hao ilibainika kuwa walikuwa wateketeze baadhi ya majengo ya shule hiyo ndipo wapate kupewa ruhusa ya kwenda nyumbani kabla ya kalenda ya Muhula.

“Wanafunzi hao walikuwa wamepanga wazue hali ya taharuki katika shule hiyo bada ya kumaliza mtihani wao wa mwisho wa muhula ili wafurushwe mapema kutoka shuleni,” akasema.

Afisa huyo alisema kuwa tayari uchunguzi wa kina umeanzishwa kubaini kama kulikuwa na mchango wa watu wengine kutoka nje ya jamii ya shule hiyo.

“Katika visa kama hizi, utapata kuwa huwa na ushawishi wa watu wengine ambao sio wadau wa shule inayolengwa na uhalifu wa aina hii. Tungetaka kujua aliyeuza petroli hiyo na kama ni wanafunzi waliiendea,” akasema.

Hatua
Bw Odende alisema kuwa tayari majadiliano yanaendelea yakihusisha wadau wa shule hiyo ili kubaini hatua itakayochukuliwa washukiwa hao.

“Ni vyema ieleweke kuwa hatua yoyote ambayo tutawachukulia washukiwa hao ni lazima iwe imeidhinishwa na wadau wa shule. Lakini kwa uhakika ni kuwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kupanga njama ya kutekeleza uhalifu,” akasema.

Aidha, alisema uchunguzi zaidi unafanywa ili kubaini kama kuna utumizi wa mihadarati katika shule hiyo.

“Mihadarati imekuwa kiini kikubwa katika utovu wa nidhamu katika baadhi ya mashule hapa nchini. Tungetaka kujua kama ni mojawapo ya kishawishi cha kupanga njama hiyo ikizingatiwa kuwa labda hata wangechoma wenzao katika mabweni,” akasema.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo