Mji wa Keroka katika kaunti ya Nyamira.
Na HENRY NYARORA,
WAFANYAKAZI watatu wa benki ya Equity
tawi la Nyamira, mwishoni mwa wiki walichomwa kwa chai moto na mteja
walipoenda kumdai mkopo wa Sh90,000 aliokosa kulipa.
Walikuwa
katika kundi la wafanyakazi watano wa benki hiyo waliosindikizwa na
mwanamke afisa wa polisi kwenda katika nyumba ya mteja huyo mjini
Nyamira walikojaribu kutwaa vifaa za elekroniki walipokumbwa na masaibu
hayo.
Mteja huyo
ambaye tunabana jina lake alisema kuwa alishtuka maafisa wa benki
walipovamia nyumba yake na kuchukua runinga na tarakilishi kwa nguvu ili
kufidia mkopo huo.
“Nilishangaa kwa nini benki iliamua kuchukua mali yangu badala ya kufidia mkopo huo kutoka kwa wadhamini wangu,” akasema.
Afisa wa
polisi alitazama mteja huyo aliye mwalimu wa shule ya msingi katika
kaunti hiyo alipowachoma wafanyakazi hao huku wenzake wawili wakitoroka
na vifaa hivyo.
Ingawa kisa
hicho kilitokea Jumamosi jioni kufikia Jumatatu, waathiriwa hawakuwa
wamepiga ripoti katika vituo vya polisi eneo hili.
Hata hivyo mteja aliyevamiwa Jumatatu alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Nyamira kuhusu tukio hilo.
Maelezo zaidi
Naibu kamisha
wa Kaunti ya Nyamira Danis Kirui alithibitisha kisa hicho na
kuwalaumu maafisa wa benki kwa kumtumia vibaya afisa wa polisi
aliyetumwa kulinda benki hiyo.
“Afisa huyo wa polisi alitumwa kulinda benki na wala sio kudai waliokosa kulipa mikopo,” akasema.
Meneja wa benki hiyo hakuwa afisini na naibu wake George Baloba alisema kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo.
Bw Baloba alikataa kueleza mwandishi wetu jinsi ya kuwasiliana na mkubwa wake ili apate maelezo zaidi kuhusu tukio hilo.