Msemaji
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Badra Masoud (kushoto)
akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam katika
ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) juu ya mikakati ya shirika hilo
katika kutekeleza miradi yake ili kupambana na tatizo la umeme nchini,
kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.
Picha na Eliphace Marwa – MAELEZO
Ndugu
zangu waandishi wa Habari napenda kuchukua nafadi hii adimu kabisa
kwangu kuweza kuzungumza nanyi siku ya leo kuelezea shughuli mbalimbali
zinazofanywa na Shirika latu la Umeme hapa nchini yaani TANESCO.
Kwanza
kabisa napenda kuwakumbusha kidogo juu ya Shirika letu lilivyokuwa
katika miaka ya 80 kwamba lilikuwa likisifika kama moja ya mashirika
bora barani Afrika, na ni ukweli usiopingika kwamba katika kipindi hicho
TANESCO ilifanya vizuri sana katika kila nyanja na hata kupata sifa
hizo. Lakini kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi na zisizo za
kiufundi mwishoni mwa miaka ya 90 shirika hili lilianza kulalamikiwa na
wateja wake kutokana na huduma kwa namna moja ama nyingine zinazodaiwa
kutoridhisha huku maeneo makuu yaliyokuwa yakiangaliwa ni ufuaji,
usafirishaji, usambazaji na uuzaji umeme.
Baadhi
ya sababu hizo ni pamoja na kukatika umeme mara kwa mara kunakotokana
na uchakavu wa miundombinu, huduma zisizoridhisha kutoka kwa baadhi ya
watendaji wa Shirika, umeme kutowafikia watanzania walio wengi hasa
maeneo ya vijijini na kasi ya kuunganisha wateja wapya kuwa ndogo.
Kutokana na changamoto hizo nilizozitaja, Shirika limeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kuboresha miundombinu ya umeme.
Maeneo yenye changamoto ya kukatika umeme
Pamoja
na ukarabati huo unaofanywa katika miundombinu yetu, yapo maeneo ambayo
umeme umekuwa unakatika mara kwa mara. Maeneo hayo ni kama vile Bahari
Beach, Kunduchi Beach, Mbezi Beach, Kimara mpaka Mbezi mwisho Mbagala,
Temeke na Kigamboni katika mkoa wa Dar es Salaam, Mererani mkoani
Arusha, Kahama, Meatu, Bariadi, Kanda ya Ziwa.
Maeneo
haya ukiangalia kwa makini utagundua kuwa miundombinu yake ilijengwa
miaka mingi na ndiyo maeneo ambayo tunawekeza nguvu kubwa zaidi
kuyaimarisha. Hivyo Shirika linapenda kuwaondoa hofu watanzania wa
maeneo hayo kuwa kukatika umeme mara kwa mara katika maeneo hayo si mgao
wa umeme na wala hakuna tishio lolote la mgao wa umeme kwa sasa, ni
matatizo yanayotokana na udhaifu katika miundombinu yetu.
Hatua ambazo TANESCO inachukua kuondoa matatizo ya umeme katika maeneo yaliyotajwa
Bahari beach:
Bahari
Beach kuna kituo kidogo cha kupooza na kusambaza umeme, kituo hiki kwa
sasa kimezidiwa baada ya kuunganishwa kuhudumia wateja wengi kuliko
uwezo wake.
Juhudi
zinazofanyika ni kuimarisha Kituo cha kupoza na kusambaza umeme
kilichopo Mbezi Beach ili kiwe na uwezo zaidi. Kazi hiyo inaendelea na
itakapokamilika tutahamisha baadhi ya wateja kutoka katika Kituo cha
Bahari Beach na kuwaunganisha kwenye kituo cha Mbezi Beach.
Mbezi Beach:
Kwenye
kituo cha Mbezi Beach ilikuwepo transfoma moja ya MVA 15, transfoma
hiyo ilishazidiwa na hivyo Shirika limeshafunga transfoma ya pili yenye
uwezo mara dufu wa ile ya kwanza, hii ina MVA 30. Ina uwezo wa kuhudumia
wateja wote wa Mbezi Beach na baadhi ya wateja tuliowahamisha kutoka
Bahari Beach na hivyo kuondoa kabisa tatizo la umeme kwa wakazi wa Mbezi
Beach na Bahari Beach.
Kimara mpaka Mbezi:
Kuna njia
moja tu ya umeme wa msongo wa kilovolti 132 inayotoka Ubungo kupitia
Kibo, Kimara, mpaka Mbezi barabara ya Morogoro. Likitokea tatizo lolote
la kiufundi kwenye njia hiyo basi linaathiri maeneo yote haya inapopita
njia hiyo.
Ili
kuondokana na tatizo hilo, Shirika linafanya utaratibu wa kujenga kituo
kingine eneo la Luguruni. Kituo hicho kitaweza kuhudumia maeneo yote ya
Mbezi mwisho na hivyo kuacha njia nyingine kuhudumia Ubungo, Kibo na
baadhi ya sehemu za Kimara. Hii itaondoa kabisa matatizo yote ya umeme
katika maeneo haya.
Kahama:
Matatizo
ya Kahama yanatokana na njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi
Kahama kuwa ndefu sana. Njia hii ina zaidi ya kilometa 200, urefu huu
kitaalamu haukubaliki kwani umeme mwingi huwa unapotea njiani kulingana
na umbali umeme huo unavyosafirishwa.
Aidha,
Shirika linaweka kituo kikubwa cha kupooza na kusambaza umeme Buzwagi
ili kufupisha njia ya kupeleka umeme kutoka Buzwagi mpaka Kahama. Kwa
kufanya hivyo matatizo ya umeme yanayowakabili wateja wa Kahama
yatakwisha ndani ya kipindi kifupi hiki.
Kanda ya Ziwa:
Kuna
matatizo yanayojirudia rudia kutokana na umeme wenye nguvu ndogo
unaotoka Mtera kupitia Dodoma mpaka Kanda ya Ziwa (low voltage).
Shirika
kwa sasa linatekeleza mradi mkubwa unaoitwa ‘Backbone’. Mradi huu
utapandisha kiwango cha umeme unaosafirishwa kutoka kilovolti 132 hadi
kilovolti 400. Makandarasi wameshapatikana na muda wowote wataanza
ujenzi, na ujenzi wa mradi huu utakapokamilika matatizo ya umeme katika
Kanda ya Ziwa yatakuwa madogo sana au yatakwisha kabisa.
Kwa
Kanda ya Ziwa hadi sasa kituo kikubwa cha umeme kilichopo Nyakato
Mwanza kimejengwa, kituo hiki kina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati
60, na umeme utakaozalishwa Nyakato utaingizwa kwenye gridi ya taifa na
kupunguza kabisa tatizo la ‘low voltage’ umeme mdogo kwa Kanda ya Ziwa.
Kituo
hiki tumekiweka makusudi ili kutoa huduma ya umeme wakati tukisubiri
upanuzi wa njia ya kusafirishia umeme katika mradi wa ‘Backbone’
ulitajwa hapo juu.
Kituo
hiki cha Nyakato kimekamilika na kitaanza kuzalisha umeme mwezi wa
Januari, 2013.
Shirika linawahakikishia wateja na wananchi wa Kanda ya
Ziwa kwamba watapata umeme wa uhakika mwezi Januari, 2013.
Mererani – Arusha:
Mererani
wanategemea umeme kutoka katika kituo cha Kiyungi kilichopo Moshi
mjini, kutoka Moshi mpaka Mererani ni kilometa 200, kwa umbali huu
kitaalamu umeme unaosafirishwa unapungua nguvu njiani.
Ili
kuondokana na tatizo hilo, TANESCO chini ya mradi wa TEDAP, imejenga
kituo cha kupooza umeme eneo la Kilimanjaro International Airport (KIA)
na sasa Mererani wanapokea umeme kutoka kituo cha KIA na mradi huu
tunatarajia kuuzindua hivi karibuni.
Temeke, Kigamboni na Mbagala:
Tatizo
la umeme la Temeke, Kigamboni na Mbagala halitokani na utendaji kazi wa
TANESCO, tatizo kubwa katika maeneo haya yanatokana na wahujumu
miundombinu ya Shirika. Kuna watu ambao hawapendi maendeleo, wanakwenda
kwenye miundombinu ambayo tayari ipo, wanaiba mafuta ya transfoma na
wanaiba nyaya za kopa. Wizi wa mafuta ya transfoma umeshamiri sana
katika maeneo haya na hii ndio sababu kubwa ya wateja wetu kukosa umeme,
kukaa gizani.
Aidha ili kuondokana na kero hii Shirika limeanza kutumia transfoma zisizo na mafuta katika maeneo hayo.
Shirika
limeweza kudhibiti hali kama hii katika maeneo ambayo wizi wa mafuta ya
transfoma ulikithiri, maeneo hayo ni kama Mbezi, Kinondoni Kaskazini na
Kawe.
Lakini
sasa wizi huu umehamiaTemeke, Shirika limefikia hatua ya kufunga aina
hii ya transfoma isiyotumia mafuta ili kupunguza wizi na uharibifu ya
miundombinu hii ambayo ni ghali sana.
MIRADI MIKUBWA ILIYO KATIKA HARAKATI ZA KUTEKELEZWA
- Watanzania wategemee nini kutoka katika miradi hii?
Mradi wa ‘City Center’ Dar es Salaam:
Kuna
mradi mkubwa unaotekelezwa kati ya Serikali ya Tanzania kupitia TANESCO
na serikali ya Finland wenye thamani ya Euro milioni 25, mradi huu upo
katika hatua za utekelezaji na utahusisha ujenzi wa kituo kikubwa cha
kupoza na kusambaza umeme katika maeneo ya katikati ya jiji na kituo
hicho kitajengwa eneo zilipo ofisi za UNICEF.
Kituo
hiki kitakapokamilika kitaweza kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme
katikati ya mji wa Dar es Salaam. Mradi huu utahusisha ujenzi wa njia ya
umeme ya msongo wa kilovolti 132 chini ya ardhi (underground cable) kwa
ajili ya kuimarisha vituo vingine vilivyopo katikati ya mji na
kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Pamoja
na kujenga nyaya za chini ya ardhi, tunategemea kuweka sakiti mzunguko
(ring circuit), mfumo ambao utasaidia kuunganisha umeme kutoka kituo
kimoja kwenda kingine iwapo kituo kimoja kitakuwa na hitilafu kwa vituo
vyote vya kupooza na kusambaza umeme jijini Dar es Salaam.
Mradi
huu tayari ameshakabidhiwa mkandarasi na ndani ya mwaka mmoja mradi huu
tunatarajia utakuwa umekamilika na umeme wa uhakika utakuwa
unapatikana.
Wakati
mradi huo ukiendelea, Shirika linapenda kuwataarifu wakazi wa jiji la
Dar es Salaam kuwa wamefunga transfoma kubwa mbili kubwa mpya katika
Kituo cha Kupooza na Kusambaza umeme cha City Center za MVA 30 na hivyo
kuimarisha upatikanaji wa umeme katikati ya jiji tofauti na ilivyokuwa
hapo awali wakati ilipoungua transfoma ya MVA 15.
Vilevile
Shirika limefunga transfoma mpya kwenye Kituo cha Kariakoo na Kituo cha
Buguruni na kurekebisha miundombinu katika kituo cha Ilala zoezi ambalo
limefanikisha kuimarika kwa hali ya upatianaji wa umeme katikati ya
jiji la Dar Es salaam ambalo mahitaji yake yamepanda kwa kiasi kikubwa
sana ukilinganisha na mwaka mmoja uliopita.
MRADI WA TEDAP
Mradi
huu wa TEDAP tumeuelezea kwa ufupi hapo juu. Kusudi kubwa la mradi ni
kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme jijini Dar na Arusha. Kwa
Arusha, mradi unaendelea na kazi zote zinafanyika Njiro. Kwa Dar es
Salaam, kazi kubwa ni kupeleka njia ya kusafirisha umeme (transimission
line) mpaka Kurasini na kujenga kituo cha kupoza umeme kutoka Kilovolti
132 mpaka kilovolti 33, njia hii itatoka Kurasini hadi Mbagala ambapo
kutakuwa na kituo kingine kikubwa cha kupoza umeme kutoka uwezo wa
kilovolti 132 mpaka kilovolti 33 na kusambaza katika maeneo hayo ya
Kurasini mpaka Mbagala.
Mradi
huu unajenga njia nyingine kubwa ya kilovolti 132 kwenda Gongo la
Mboto, ambapo kitajengwa kituo kingine kikubwa cha kupooza kutoka uwezo
wa kilovolti 132 mpaka kilovolti 33 na kuunganisha hiyo sakiti na kituo
cha Kipawa.
Kwa
ufupi ni kwamba kutakua na sakiti mzunguko (ring circuit) kutoka Ubungo
– Kurasini – Mbagala hadi Gongo la Mboto na kurudi Kipawa.
Mzunguko
huu utatuhakikishia umeme wa uhakika kwa jiji zima la Dar es Salaam.
Kama umeme ukikosekana eneo moja ni rahisi kuunganisha kwa kupitia
upande wa pili na umeme ukaendelea kupatikana.
Hata
hivyo kuna baadhi ya vituo vya zamani ambazo uwezo wake umekua
ukipungua kadri mahitaji yalivyokuwa yanazidi kuongezeka. Vituo hivi ni
kama vile Kituo cha Kipawa ambacho kwa sasa Shirika linafunga transfoma
kubwa mbili zenye uwezo wa MVA 90, kazi hii itakamilika ndani ya mwezi
mmoja, wananchi wanaokaa maeneo ya Tabata, Kisarawe na Gongo la mboto
tayari watakua na uhakika wa umeme.
Umeme
wa maeneo haya yaliyotajwa unatoka Ilala, na pale kazi hii ya Kipawa
itakapomalizika, umeme wa maeneo haya utakuwa unatoka Kipawa ambapo ni
karibu na maeneo hayo na umeme utakua ni wa uhakika zaidi.
Aidha
tumefunga transfoma mbili kubwa katika Kituo Kikuu cha Kupooza na
Kusambaza umeme cha Ubungo ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa
upatikanaji wa umeme kwa jiji la Dar es Salaam.
MIRADI YA UZALISHAJI
Kwenye upande wa UZALISHAJI WA UMEME:
Mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara – Dar es Salaam
Wakati
ujenzi wa bomba unaendelea TANESCO kwa kushirikiana na serikali
inajitahidi kuhakikisha kuwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia
gesi hiyo inakuwa tayari.
Kwa
sasa tayari kuna mitambo mingi inayozalisha umeme kwa kutumia gesi
asilia nyingi tofauti na kiwango cha gesi kinachozalishwa.
Mradi wa Kinyerezi
TANESCO
ina mashine zenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 150 zinazotumia
gesi ambazo hatuwezi kuzitembeza kwa sababu hatuna gesi. Bomba
litakapofika, pamoja na kuendesha mashine ya megawati 150 lakini pia
tunaanza utaratibu wa ujenzi wa vituo ifuatavyo:
o Tutakua
na mtambo wa megawati 150 utakaojengwa Kinyerezi na taratibu za ujenzi
wa mtambo huu zimeshaanza na muda sio mrefu jiwe la msingi litawekwa.
o Tutakua na mradi wa meagawati 240, Megawati 300 na megawati 300 ambayo yote itajengwa pia Kinyerezi.
Hii
miradi itakapomilika kati ya mwaka mmoja hadi miwili ijayo. TANESCO
itakuwa na uhakika wa umeme usiopungua megawati 990 zinazotokana na
gesi.
Mradi wa Kilwa Energy
Tuna
mradi Kilwa, mradi huu unaitwa Kilwa Energy ukikamilika utatoa uhakika
wa megawati 320, ni mradi wa mwekezaji binafsi na Shirika liko kwenye
mazungumzo kuhakikisha mchakato wa mradi huu unakamilika. Bahati nzuri
mazungumzo yamefikia hatua nzuri. Mradi huu utajengwa Kilwa na
utaambatana na ujenzi wa njia ya msongo wa 240MV ‘double circuit
line’ kutoka Kilwa mpaka Dar es Salaam.
Mradi
wa kujenga mtambo wa umeme wa megawati 600 mkoa wa Mtwara utajengwa na
Kampuni ya Symbion ya Marekani na kusafirisha umeme hadi Songea na
Makambako na hatimaye kuunganishwa katika Grid ya taifa.
MIPANGO YA MIRADI YA USAFIRISHAJI
Ukijenga tu miradi hii ya kuzalisha umeme bila kujenga njia za kusafirisha umeme huo utakuwa haujakamilisha kazi.
Mipango
iliyopo kwenye mikakati na ambayo imeshaingizwa katika mipango ya
kitaifa ya kurekebisha miundombinu ya umeme ni pamoja na hii ifuatayo:
o Mradi
wa ‘North East Grid Transmission Line’ ya kutoka hapa Ubungo kwenda
hadi Arusha, mradi una nia ya kuimarisha miundombinu ya umeme Kanda ya
Kaskazini, Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha , mradi huu ni muhimu
sana kwa sasa hivi ukiacha Kanda ya Ziwa ambapo ‘Backborne Projects’
imeanza kutekelezwa eneo lingine ambalo miundombinu yake ni dhaifu sana
ni Kanda hii ya Kaskazini na upotevu mwingi wa umeme unatoka huko.
o Pia
TANESCO kwa kushirikiana na ufadhili wa serikali ya Sweden chini ya
shirika lake la SIDA, Shirika linaanza utekelezaji wa mradi kutoka
Makambako mpaka Songea.
Mwanzoni kulikuwa na mpango wa kuweka mradi wa
kujenga njia ya kilovolti 220 mpaka Madaba na kilovolti 132 kutoka
Madaba mpaka Songea. Sasa hivi baada ya kuona maendeleo kwenye makaa ya
mawe hasa maeneo ya Ngaka na Mchuchuma, tumeona ni vyema kuupanua mradi
huu na kujenga njia ya kilovolti 220 badaala ya 132 kutoka Makambako
hadi Songea. Mkandarasi ataanza kazi hii kabla ya mwisho wa mwaka huu.
o Mradi
mwingine wa usafirishaji umeme ambao upo katika hatua za utekelezaji ni
mradi wa ‘North West Grid’ – ambao utasaidia upatikanaji wa umeme wa
uhakika kwa utatupa sasa uhakika kwa mikoa wa Mbeya, Rukwa na Katavi,
Mpanda , Kigoma , Nyakanazi na kurudi kuunganisha na Kahama. Mradi huu
ni muhimu sana, kwa kuwa utakapokamilika nchi nzima itakuwa
imeunganishwa kwenye gridi ya Taifa.
o Mwisho
kabisa maeneo ya Lindi na Mtwara hayajasahaulika, tuna mipango mingi.
Tunategemea Mtwara kuwa na mtambo wa megawati 320 ambao utaunganishwa na
njia ya kusafirisha umeme ‘transmission line’ mpaka Kilwa, Lindi. Kituo
hicho pamoja na kujengwa kwa kituo hicho kitaunganishwa na gridi ya
Taifa ya kutoka Mtwara kupitia Somanga na kutoa umeme Somanga na
kuuleta Dar es Salaam.
Kwa
mikakati hii tutakua na uwezo wa kutoa umeme Mtera na Kihansi na
kuupeleka Kigoma, Mpanda n.k. na nchi nzamia itakua imeingizwa katika
gridi ya Taifa.
Tunasisitiza kwamba miradi yote tuliyoieleza ni ya uhakika kwa kuwa taratibu za utekelezaji zimeanza kufanyika.