Kutokana na wajumbe wa baraza la wawakilishi kutoa shtuma nzito juu
ya utendaji wa wizara ya mindombinu na mawasiliano ya Zanzibar ,spika wa
baraza la wawakilishi ameamua kuahirisha mjadala wa wizara hiyo ili
kuwapa muda zaidi waziri na watendaji wake kujipanga na kuja na majibu
ya uhakika.
Hatua hiyo imekuja baada ya wajumbe wa baraza hilo kutoka CCM na
CUF wapatao zaidi ya 50 kuchangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo
iliyowasilishwa na waziri wa miundombinu na mawasiliano Mhe Rashid Seif,
ambapo karibu wajumbe wote walikuwa wakali na kutoridhika na utendaji
wa wizara hiyo katika masuala ya utawala,ujenzi wa viwanja vya ndege na
uimarishaji na ujenzi wa barabara za Unguja na Pemba ,usafiri wa
baharini ambapo wajumbe waliweka misimamo yao ya kuzuia vifungu na
kutoa shilingi wakati wamajumuisho.
Kutokana na hoja hizo za wawakilishi Spika alisogeza mbele mjadala
huo na kuamua wizara ya biashara kuwasilisha bajeti yake huku waziri wa
mindombinu anatarajiwa kujibu hoja za wawakilishi baada ya wizara ya
biashara kumaliza uwasilishaji wake.