Mkurugenzi
wa Mipango na Matumizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Bw.
Valentine Msusa akijibu swali la mwandishi wa Habari kuhusu maboresho ya
makusanyo ya mapato ya Serikali kwenye sekta ya Misitu, wakati wa
mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dar
es Salaam. Kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bw Frank
Mvungi.
Moja
ya Mradi wa misitu unaosimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania ambao ni
chanzo cha mapato ya Serikali.(PICHA ZOTE NA GEORGINA MISAMA-MAELEZO).
Wakala wa
Huduma ya Misitu Tanzania katika kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa
sasa (Big Results Now), pamoja na Sera ya Misitu ambayo inasisitiza
katika kuhakikisha uendelezaji endelevu wa misitu, umefanya maboresho
katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka
na kuongeza udhibiti wa uvunaji na ukusanyaji wa mapato. Maeneo
yaliyofanyiwa maboresho ni pamoja na;
1. Kufanya mapitio ya bei ya mazao ya misitu,
2. Kufanya mapitio ya Mwongozo wa uvunaji endelevu wa misitu wa mwaka 2007,
3. Uuzaji wa miti ya Misaji (Teak) kwa njia ya mnada na
4. Kuimarisha ulinzi katika vizuia na kusitisha ukusanyaji wa maduhuli katika vizuia hivyo.
Kuanzia
tarehe 14/09/2013 ukusanyaji wa tozo, faini na malipo yo yote ya fedha
kwenye vizuia umezuiliwa. Mazao yoyote yatakayokutwa sio halali au
nyaraka zake zina mapungufu gari litazuiwa katika kizuia na mhusika
atapaswa kulipa faini katika vituo vilivyoteuliwa kufanya kazi hiyo.
Mazao yaliyozidi au kutokuwa na nyaraka halali yatateremshwa na
kutaifishwa.
Katika kufanya maboresho hayo wakala umefanya yafuatayo:
(i) Mapitio ya bei ya mazao ya misitu
Bei za mazao ya misitu zitapandishwa kwa kuzingatia utafiti uliofanywa na mshauri mwezeshaji ambaye amezingatia
-gharama za uzalishaji wa miche ya miti hadi kufikia hatua ya kuvunwa,
-kupanda kwa gharama za huduma na vifaa vya uzalishaji na kiwango cha ubadilishaji wa fedha ya Tanzania, na
-Kupanda kwa Gharama za vibarua na wafanya biashara wanaotoa huduma katika mashamba ya miti
Maboresho hayo yatapunguza hasara ambayo Serikali inapata kutokana na kuuza mazao ya misitu kwa bei ya chini.
(ii) Kufanya mapitio ya Mwongozo wa Uvunaji Endelevu wa Misitu wa mwaka 2007.
Maeneo yaliyoboreshwa ni pamoja na
-Kuandaa Miongozo miwili tofauti iliyotayarishwa kwa ajili ya Mashamba ya Miti na Misitu ya Mikoko na ule wa Misitu ya Asili.
-Kuboresha takwimu za hali ya misitu hapa nchini na
-kuweka Masharti ya viwanda vya kuchakata mazao ya misitu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Misitu ya mwaka 2002.
Mwongozo huu unawaelekeza wadau na wananchi kwa ujumla juu ya;
-utaratibu wa kuvuna,
-usimamizi na kufanya biashara ya mazao ya misitu,
-masharti ya kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya misitu,
-masharti ya kufanya biashara ya mazao ya misitu ndani na nje ya nchi,
-nyaraka mbalimbali zinazokubalika kisheria wakati wa kuvuna,
-kusafirisha na kufanya biashara ya mazao ya misitu,
-utaratibu wa namna vijiji vinavyopakana na misitu vitakavyonufaika na misitu inayowazunguka.
(iii) Uuzaji wa Miti ya Misaji (Teak) kwa Njia ya Mnada
Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania, ulianza kutekeleza uuzaji wa mazao ya misitu
kwa mnada mwaka 2012/2013. Zoezi hili limetekelezwa kwenye Mashamba ya
miti ya Misaji (Teak) yaliyopo Longuza, Mtibwa na Rondo. Matokeo mnada
huo yalikuwa mazuri na tulipata ongezeko la bei kwa asilimia (66%) kwa
kila mita ya ujazo. Hivyo uzoefu huu unaonyesha kuwa uuzaji wa miti kwa
njia ya mnada unaleta matokeo makubwa kuliko njia nyingine.
Pamoja na
faida hiyo imeonekana mnada una gharama ndogo za kiutawala, uwazi, na
unatoa fursa kwa wavunaji wadogo na wakubwa kushiriki. Aidha, zoezi la
uaandaaji wa mnada unachukua muda mfupi. Katika Mashamba ya miti laini
(softwood) ya kupandwa, maandalizi ya utaratibu wa mauzo, yatazingatia
uzoefu wa mnada wa miti ya misaji na uamuzi utafanyika baada ya
kufanya utafiti wa kutosha.
(iv) Kuimarisha Ulinzi Katika Vizuia Na Kusitisha Ukusanyaji Wa Maduhuli Katika Vizuia Hivyo.
Wakala
umeamua kusitisha ukusanyaji wa tozo, faini, na malipo yoyote ya fedha
kwenye Vizuia vya ukaguzi wa mazao ya misitu na hivyo vitafanya kazi ya
ukaguzi tu ili kuhakiki kama mazao yanayosafirishwa yamelipiwa ushuru na
tozo nyingine na kama yana nyaraka halali.