Na Eliphace Marwa – MAELEZO
SERIKALI kupitia Wakala wa Uchimbaji Visima na
Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) imepanga kuchimba visima virefu 300 vya maji
katika mwaka wa fedha wa 2013⁄2014 katika maeneo mbalimbali nchini ili
kupambana na tatizo la maji nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Idara ya
Habari – MAELEZO jijini Dar es Salaam Ofisa Masoko wa Wakala hiyo Nungu
Egwagwa alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013⁄2014 Wakala
imejipanga kuwafikia wananchi mahali popote walipo na kuwapatia huduma
sahihi na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kukabiliana na soko la
ushindani.
″Wakala inajitahidi kutoa elimu kwa wananchi juu ya viwango
vinavyotakiwa wakati wa uchimbaji visima ili kuweza kupambana na
ushindani ulioko sasa ambapo wachimbaji binafsi walio wengi kutozingatia
viwango vya ubora wakati wa uchimbaji hivyo kufanya gharama zao
kuonekana nafuu ukilinganisha na za Wakala,″ alisema Nungu.
Aidha wakala imebainisha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo hivi
sasa ikiwemo tatizo la mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuongezeka kwa
gharama za uchimbaji kutokana na maji kupatikana katika umbali mrefu.
Pia Wakala imebainisha kuwa uchakavu wa mitambo wanayotumia
imechangia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji ila katika mwaka wa
fedha wa 2013⁄2014 Wakala imejipanga kutoa huduma bora zaidi kwa
kuwatumia wataalamu wao na vifaa vya kisasa zaidi ili kuongeza ufanisi
katika uchimbaji visima.
Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ulianzishwa
mwaka 1997 ambapo toka Januari 1997 mpaka Juni mwaka huu wamechimba
jumla ya visima 6929 na visima 5899 ambayo ni sawa na asilimia 85 ya
mafanikio.