Na Magreth Kinabo – MAELEZO
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Seith Kamuhanda amempongeza Rais Jakaya Kikwete
kwa kuwateua viongozi ambao ni majembe (wachapakazi) kuiongoza wizara
hiyo huku akisema ni watendaji wenye uwezo wa hali ya juu.
Viongozi walioteuliwa kuongoza wizara hiyo ni Sihaba Nkinga ambaye ni
Katibu Mkuu wa sasa na Naibu Katibu Mkuu wake ni Profesa Elisante ole
Gabriel Laizer.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kamuhanda wakati akiwaga viongozi wa
wizara hiyo ambapo pia aliwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa
ushirikiano ili kuhakikisha huduma wanazozitoa kupitia sekta za habari,
vijana, utamaduni na michezo zinawafikia wananchi.
“Leo ni siku ya furaha kwangu kwa sababu ninaacha majembe mawili ya
uhakika. Ninawaomba muwape ushirikiano ili walime vizuri. Ni wizara
ngumu kwa sababu inagusa Watanzania wote,” alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa sasa Sihaba alisema anamshukuru
Kamuhanda kwa kumfundisha kazi katika maeneo mbalimbali ya sekta za
wizara hiyo.
“Nimekaa katika kiti hiki bila ya yeye nisingeweza kukaa katika kiti
hiki bado ataendelea kuwa msaada kwangu kwa kuwa wizara inagusa jamii,”
alisema Katibu Mkuu Sihaba huku akimwomba aendelee kutoa msaada katika
wizara hiyo.
Aidha Katibu Mkuu huyo alisema atajitahidi kuongoza wizara ili
iendelee kuwa watoto wa familia moja kama ilivyoachwa na Kamuhanda. Naye
Naibu Katibu Mkuu Profesa Laizer alisema anamshukuru Kamuhanda kwa
ushirikiano aliowapo, pia aliongeza kuwa kufanya kazi kwake vizuri
kutokana na ushirikiano huo ukiwemo wa wakurugenzi, viongozi wa taasisi
na watumishi wa wizara hiyo.
“Kazi kubwa niliyonayo ni kumsaidia Katibu Mkuu. Nitawasaidia ili
tupate Matokeo Makubwa Sasa. Tutajitahidi tusikuangushe,” alisisitiza
Profesa Laizer huku akisema wao ni majembe lakini yeye ni shoka na
ametoka katika wizara hiyo kwa heshima.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya menejimenti ya wizara hiyo
Profesa, Hermans Mwansoko alimpongeza Kamuhanda kutokana na utendaji
kazi wake wakati akiiongoza, ambapo alisema ameiacha katika hali ya
umoja na mshikamano huku akiwajali watumishi hususan wa ngazi za chini.