Mugabe ashinda uchaguzi wa urais wa Zimbabwe
Kwenye sherehe ya kuapishwa kwake, rais Mugabe alisema anapenda kufanya mazungumzo na chama cha
upinzani.
Vile vile atahudhuria mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika unaofanyika tarehe 29 Juni na tarehe mosi Julai nchini Misri, ambapo atatafuta maelewano na uungaji mkono kutoka nchi za Afrika katika juhudi za kuondoa msukosuko uliopo sasa nchini Zimbabwe.
Duru la pili la upigaji kura wa uchaguzi wa urais lilifanyika tarehe 27 Juni nchini Zimbabwe. Kabla ya hapo mgombea mwingine Bw. Morgan Tsvangirai kutoka chama cha upinzani cha MDC alitangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo. Kutokana na hali hiyo, nchi nyingi zilikuwa zikiishauri Zimbabwe iahirishe upigaji kura, lakini Zimbabwe haikukubali pendekezo hilo na kufanya upigaji kura kama mpango uliowekwa.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi huo wa urais, Bw. Mugabe mwenye umri wa miaka 84 aliapishwa kuwa rais wa awamu ya 6 wa Zimbabwe, na anaendelea kuchukua wadhifa huo tangu Zimbabwe ipate uhuru mwaka 1980.
Hivi sasa serikali ya Zimbabwe inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, kutokana na nchi nyingi kutilia shaka uhalali wa upigaji kura wa duru la pili. Ili kuondoa msukosuko huo, rais Mugabe alieleza kufurahia usuluhishi wa rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, ambaye ni msuluhishi wa msukosuko wa Zimbabwe aliyeteuliwa na jumuiya ya SADC.
Rais Mugabe alieleza bayana kuwa, anapenda kufanya
mazungumzo na chama cha upinzani, pia alitoa wito kwa vyama mbalimbali
vya kisiasa nchini Zimbabwe vikae pamoja na kufanya mazungumzo.
Alisisitiza kuwa kufanya mazungumzo ya dhati kati ya vyama mbalimbali
vya kisiasa ni njia mwafaka ya kutatua matatizo.
Pamoja na kutoa wito huo, rais Mugabe pia alitoa masharti ya kufanya mazungumzo. Waziri wa sheria wa Zimbabwe Bw. Patrick Chinamasa alitoa ufafanuzi kuhusu masharti hayo, akisema mazungumzo hayo yatafanyika kati ya vyama viwili tu, yaani chama tawala cha Zanu-PF na chama cha upinzani MDC, upande wa tatu haupaswi kuingilia kati, aidha masuala kuhusu mgawanyo wa mashamba na ukosoaji dhidi ya mageuzi ya ardhi hayapaswi kujadiliwa kwenye mazungumzo hayo, na chama cha MDC kinatakiwa kushirikiana na chama cha Zanu-PF katika kuiomba jumuiya ya kimataifa iondolee vikwazo Zimbabwe.
Kiongozi wa chama cha MDC Bw. Morgan Tsvangirai hakujibu mara moja wito huo. Hatua ya kwanza aliyochukua ni kukataa kukubali matokeo ya upigaji kura wa duru la pili, akisema huu ulikuwa ni mchezo wa kuchekesha watu, na Bw Mugabe alipata kiti cha urais kwa njia isiyo halali. Baadaye Bw. Tsvangirai alisema anaweza kukubali kufanya mazungumzo na chama tawala, lakini hatafanya mazungumzo na serikali haramu.
Kauli hizo zinaonekana kukinzana, lakini kutokana na hali ilivyo
sasa nchini Zimbabwe, kuna uwezekano mkubwa kwa chama tawala cha
Zanu-PF na chama cha upinzani cha MDC kufanya mazungumzo.
Nchi nyingi za magharibi zimeghadhabishwa sana na kuchaguliwa tena kuwa urais kwa Bw. Mugabe, zimetangaza kuiwekea Zimbabwe vikwazo vikali zaidi, na zitakabidhi suala la Zimbabwe kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Afrika zimesema, vikwazo dhidi ya Zimbabwe haviwezi kuondoa msukosuko wa hivi sasa, bali vitawaumiza zaidi watu wa nchi hiyo.
CHANZO:BBC