(Kutoka kushoto) Samson Wachira na mkewe Maureen Chebet, Peter Mbugua na mkewe Charity Nyokabi, Stephen Kinyanjui na mkewe Patricia Wanjiru, Herman Gakobo na mkewe Zipporah Wambui, George Wango na mkewe Penninah Wanjiru wakati wa harusi yao kanisa la St Peters, Kiratina mjini Nakuru Agosti 3, 2013. Picha/SULEIMAN MBATIAH
Na RACHEL KIBUI
KULIKUWA na shangwe na vigelegele katika kanisa moja viungani mwa mji wa Nakuru Kenya wakati ndugu watano walipofunga pingu za maisha wakati mmoja.
Harusi hii ya
kipekee ilifanyika katika kanisa katoliki la mtakatifu Peter katika
mtaa wa Kiratina karibu na barabara kuu ya kutoka Nakuru kuelekea
Nairobi.
Maharusi waliojawa na furaha isiyo na kifani walielezea kuwa malezi yao bora yaliwafanya kuonelea vyema kufunga ndoa siku moja.
Kulingana na
Samson Wachira, ambaye ni kifunguamimba, wazazi wa vijana hao
waliwaonyesha kupendana na kushirikiana katika mambo yote.
Hivyo basi, Wachira alielezea, kila mmoja wao alipotaka kufunga ndoa rasmi, aliwaita nduguze kwa ushauri.
Wachira ana mika 36 ilhali George Wango, ambaye ni kitindamimba ana umri wa miaka 24.
Wengine walikuwa Peter Mbugua, 35, Stephen Kinyanjui, 34, na Harman Kago,32.
Ndugu hao waliitaja siku hiyo kama ya furaha ambayo wamekuwa wakiingojea kwa hamu na ghamu.
“Tumekuwa tukiingoja na kujitayarisha kwa siku hii kwa mwezi mmoja uliopita,” alisema Wango, ambaye ni mwanajeshi.
Wazo la
kufunga ndoa siku moja liliwajia ndugu hao miezi saba wakati kasisi
mmoja alipowatembelea nyumbani mwa baba yao katika eneo la Kiratina.
Baba yao
alikuwa ameandaa karamu na ibada ya misa ya shukrani wakati kasisi
alitaka kujua ni nani kwa familia hiyo alikuwa amekubaliwa kupokea
sakramenti.
Kulingana na
desturi za kanisa la Katoliki, ni sharti mwanamume awe amefunga ndoa
rasmi kanisani ili kuruhusiwa kupokea sakramenti.
“Kasisi huyo aliwapa changamoto vijana hao kuhusu faida za kufunga ndoa kanisani.”
Baada ya kushauriana baina yao, vijana hao walienda kuomba mawaidha kutoka kwa baba yao Bw James Kago.
Kuwaunganisha
“Niliwahimiza
wafunge ndoa siku moja kwani hii ingewawezesha kufanya haraka,
kupunguza gharama na zaidi ya hayo kuwaunganisha,” alisema Bw Kago,
ambaye ni mwanajeshi aliyestaafu.
Kwa mwezi
mzima uliopita, mzee huyo na jamii yake wamekuwa wakienda kwa wazazi wa
wake za kila kijana mmoja baada ya mwingine ili kupeleka mahari na
kuomba idhini ya kufunga ndoa rasmi.
Kinyume na wengi, bi harusi waliokuwa wakiolewa walimsifu sana mama mkwe hasa kwa kuunga mkono ndoa hizo na kuwashauri.
“Mama mkwe
amekuwa akitushauri jinsi ya kukaa kwa amani na kutilia maanani upendo
kwa nyumba zetu,” alisema Bi Maureen Chebet, mmoja wa bi harusi
Chebet alisema kuwa wakwe zake wamekuwa wakiwaonyesha upendo kama tu wa mama mzazi.
Naye Bi
Elizabeth Wambui, ambaye ni mama ya vijana waliokuwa wakifunga ndoa,
alisema kuwa alionelea vyema wafunge ndoa siku moja kama njia ya
kuwaunganisha wana wake.
“Hii ni siku ambayo kama jamii hatutasahau kamwe, watoto wangu wote sasa ni kama mapacha,” alisema mama huyo.