Dar
es Salaam.
Wakati matukio ya baadhi ya vigogo na wasanii maarufu
wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulenya hayajapoa,
imebainika kuwa mtambo maalumu wa kuchanganya na kuziongezea thamani
dawa hizo upo hapa nchini.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa mtambo huo ambao awali ulikuwa
unapatikana Mombasa, Kenya, pekee, unatumika kuchanganya dawa za
kulevya na kemikali nyingine ambapo nusu kilo ya heroine huongezwa hadi
kufikia kilo mbili. Uchunguzi
unaonyesha kuwa kuwa mtambo huo ulioingizwa mwaka huu na kigogo mmoja wa
dawa hizo, upo katika nyumba moja iliyopo eneo la Mbezi Beach.
Mmoja
wa watumiaji wa dawa hizo ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kuhofia
usalama wake, alisema mtambo huo umerahisisha upatikanaji wa heroine
nchini maarufu ‘white sugar’ kama inavyojulikana mitaani.
“Zamani
‘white sugar’ ikitoka shamba (nchi inakotengenezwa yaani Pakistan na
nchi nyingine) ilikuwa inapelekwa Mombasa, Kenya, ambako kuna mtambo wa
kuchanganya na dawa nyingine ili iongezeke wingi wake, lakini kazi hiyo
inafanyika hapa hapa nchini kwa sasa,” alisema.
Alipoulizwa
kuhusu uwepo wa mtambo huo hapa nchini, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa
za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema kuwa kuna taarifa alizonazo ambazo
bado anazifanyia kazi.
“Hata kama nikiwa nazo nazifanyia kazi, za kwangu mimi nazifanyia kazi na hata za kwako nazifanyia kazi,” alisema Nzowa.
Hata
hivyo, Nzowa akizungumza katika kipindi cha Malumbano ya Hoja
kilichorushwa na Televisheni ya ITV juzi, alisema kuwa katika siku za
hivi karibuni wafanyabiashara wa heroine wamekuwa wakiingiza nchini
malighafi za dawa hizo, tofauti na awali ambapo walikuwa wakiingiza dawa
hizo zikiwa tayari kwa matumizi.
Akitoa
mfano alisema kuna raia wa kigeni alikamatwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akiwa na malighafi
hizo zilizokuwa zikifanana na sukari na kwamba Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) na Mkemia Mkuu wa Serikali, ndiyo waliobaini kuwa haikuwa
sukari kama ilivyodhaniwa.
Alisema
kutokana na uhaba wa dawa hizo bei ya kete imepanda ambapo hivi sasa
hakuna kete ya gramu 0.11 inayouzwa chini ya Sh 3,000.
Hii ni
mara ya pili kubainika kuwepo kwa mtambo wa kutengenezea dawa za
kulevya nchini. Miaka ya hivi karibuni jeshi la polisi lilikamata mtambo
wa kutengenezea dawa za kulevya katika nyumba moja iliyopo eneo la
Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi
uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya kuwepo mtambo huo kuna nyumba tano
katika eneo la Tandika jijini Dar es Salaam karibu na soko, ambazo
zinatumika kuuza dawa za kulevya huku baadhi ya polisi wa Mkoa wa
Kipolisi wa Temeke, wakiwalinda wauzaji wake kwa kuwapa taarifa ya
mipango inayopangwa na jeshi la kuwatia mbaroni.
SOURCE:MWANANCHI.CO.TZ
