Bw. Fungo Kamili ambaye ni mlemavu wa mguu, akimwonesha mwandishi wetu miti aina ya mianzi ambayo anaitumia kwa shughuli za utengenezaji wa samani
Mara nyingi tumeshuhudia katika jamii watu mbalimbali wenye ulemavu hasa wa viungo wakiwa na mawazo kuwa wao ni watu wakutegemea kutoka kwa watu wengine hasa ambao hawana ulemavu, kwa madai kuwa wao hawawezi chochote zaidi ya kuomba
Na kutokana na kuomba huko kwa kuwa ni hiari ya mtu, wengi wamekuwa wakipata misaada michache ama wakati mwingine kupewa msaada mkubwa lakini hawawezi kusema kuwa wametosheka na badala yake zoezi hilo la kuwa tegemezi linazidi kushika kasi kwao
Ulemavu hutofautiana baina ya mtu mmoja na mwingine, hapa kwa leo nazungumzia walemavu wale ambao ulemavu wao unawaruhusu kujishughulisha na baadhi ya kazi ambazo zinawaingizia kipato kikubwa kuliko hata wanavyodhania
Bw. Fungo Kamili ni mlemavu wa mguu kutoka wilaya ya Makete mkoani Njombe ambaye alikuwa na mawazo ya kuwa tegemezi toka awali lakini kutokana na ubababishaji uliopo kwenye utegemezi kutoka kwa baadhi ya watu na hata mashirika aliyokuwa akidhania kuwa ni msaada kwake, hivi sasa ameamua kuondokana na utegemezi huo na kuamua kujishughulisha na kazi ambayo inamuingizia kipato kinachomsaidia kuendesha familia yake
Fungo amesema alikuwa anafanya kazi kwenye shirika fulani hapa Makete(jina tunalihifadhi) ambalo lilimkabidhi kitengo cha karakana ya ufundi uashi ambapo kutokana na juhudi zake kitengo hicho kilikuwa kikiingiza zaidi ya milioni 30 kwa mwezi, lakini mshahara wake ulikuwa 80,000/= kwa mwezi, hata kama mapato hayo yataongezeka ama lah
Kutokana na ongezeko hilo la mapato aliamua kuwaomba wahusika wamuongezee mshahara kwa kuwa anayaona mapato anayoingiza ni mengi lakini hakuna aliyeonesha kumjali na badala yake walimpa maneneo matamu ya kumsihi awe mvumilivu ipo siku ataongezewa lakini kila akikumbushia ahadi hiyo aliambulia kupata maneno badala ya vitendo
Kufuatia hali hiyo aliamua kuomba likizo ya bila malipo ya miezi mitatu na hakurudi tena hapo kazini na badala yake aliamua kujiingiza kwenye shughuli binafsi za kutumia ubunifua wake ambazo zilimuingizia fedha za kumtosha tangu alipoacha kazi hadi hivi sasa
Kama ilivyoa ada kuwa kama utaamua kuumiza akili kuwa ufanye shughuli gani ikuingizie kipato kwa haraka na uhakika basi lazima iwe hivyo, kitu ambacho alikifanya Fungo Kamili na kumpa ahueni ya maisha hadi hii leo
miti aina ya mianzi
Wilaya ya Makete ina miti aina ya mianzi ambayo imegawanyika katika makundi ya aina mbili, aina ya kwanza hutumika kwa ajili ya kutengeneza pombe ya kienyeji aina ya ulanzi ambayo ni maarufu sana katika mkoa wa Njombe na Iringa na kundi la pili ni mianzi migumu ambayo hutumika kutengenezea samani mbalimbali (shughuli za ujenzi), hivyo Fungo aliamua kujiingiza kutengeneza samani mbalimbali kwa kutumia miti aina ya mianzi
Miongoni mwa vitu anavyotengeneza ni nyungo, vimikebe, vibakuli, makochi/viti vya kukalia na vingine vingi ambavyo huvitengeneza kwa wingi na soko lake kubwa ni wazungu ambao hufika mara kwa mara kwenye kituo alichokuwa akifanyia kazi awali na kuacha kazi baada ya kuona haina maslahi, na kwa kuwa wanamfahamu basi humpa 'oda' ya vitu ambavyo wanavitaka na yeye huwatengenezea kazi anayoifanyia nyumbani kwake
Baadhi ya samani anazotengeneza
Kutokana na kufanya shughuli hii ambayo anaipenda na kuitegemea amesema humpatia zaidi ya laki tatu kwa mwezi kama biashara ikiwa mbaya, lakini ikiwa nzuri humpatia hadi laki sita kwa mwezi, fedha ambazo huzitumia kusomesha watoto pamoja na kuendesha biashara hiyo na hata shughuli zingine zozote zinazojitokeza
Bw. Fungo anatoa wito kwa walemavu kote nchini kufanya kazi kulingana na ulemavu alionao na kuacha dhana potofu kuwa wao ni watu wa kusaidiwa tu, kwani kwa kufanya hivyo kutamkwamua na makali ya maisha yaliyomzonga
"Kuna mtu utakuta hana mkono mmoja umelemaa halafu anakaa na kutegemea kwenda kuwa omba omba, zipo kazi anazoweza kuzibuni na kuzifanya zikamuingizia hela nyingi tu, cha msingi walemavu tuwe wabunifu, tutatoka kimaisha"alisema Fungo
Na Eddy Blog