Wananchi wa kata ya kitulo wilaya ya Makete mkoani Njombe wamehakikishiwa kupata umeme na maji ifikapo Desemba mwaka huu
Kauli hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Makete ambaye pia ni naibu waziri wa maji Dk Binilith Mahenge katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo katani hapo
Dk Mahenge amesema tayari transfoma ya kwa ajili ya umeme wa kata hiyo imeshapatikana na ipo katika ofisi za tanesco wilaya ya Makete na itafungwa mwezi huu hivyo waondoe shaka
"Najua tabu mnazozipata kwenye suala zima la umeme hapa Kitulo lakini litakwisha hivi karibuni maana mwezi huu Tanesco watakuja kufunga transfoma hapa na taratibu zingine zifuate lakini hadi desemba mwaka huu umeme lazima uwake" alisema Mahenge
Kwa upande wa maji amesema tayari mkandarasi ameanza kutengeneza inteki (njia ya maji) ili wananchi waanze kupata maji ya bomba baada ya kupata adha ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu
Nao wananchi wa kata hiyo wamesema wamefurahishwa na maneno hayo na kumtaka mbunge kufuatilia masuala hayo kwa makini huku wakimpongeza kwa kuwatembelea na kusikiliza kero zao na kuzipatia majibu
Na Riziki Manfred