Barabara ya Samora katikati ya jiji la Dar es Salaam imefungwa kwa
saa kadhaa huku jeshi la polisi likiimarisha ulinzi katika maeneo yote
ya mtaa huo ili kufanikisha zoezi la kuwaondoa wapangaji waliokuwa
wakiishi katika baadhi ya nyumba za shirika la nyumba la taifa zilizopo
katika mtaa huo.
Zoezi la kuwaondoa wapangaji hao katika nyumba hizo
ambazo ni mali ya shirika la nyumba la taifa ilianza tangu saa 12
asubuhi sambamba na zoezi la ubomoaji uliofanywa na tingatinga huku
zoezi hilo likisimamiwa na askari wa jeshi la polisi ili kuakikisha
linafanikiwa kama hivi.
Baadhi ya wapangaji hao,akiwemo bwana Anely Chawda
na Bi Debora Kamboge, wamelalamikia uongozi wa shirika la nyumba la
taifa kwa kukiuka mkataba waliowapa kwa kusema mkataba huo ulitakiwa
kuisha mwezi Novemba mwaka huu kwa mujibu wa mkataba wa shirika la
nyumba la taifa walivyoandika wenyewe,lakini cha kusikitisha zaidi ni
kwamba mpaka mwezi huu wa August 2013 walilipa kodi katika shirika hilo
na ikapokelewa na risiti wanazo lakini wameondolewa katika nyumba hizo
bila kujua wataenda kuishi wapi na shughuli zao watafanyia wapi.
Wakala wa shirika hilo bwana Joshua Mwaituka,
aliyekuwepo eneo la tukio, alionekana kuzingirwa na baadhi ya wapangaji
hao kwa lengo la kuhoji kwa nini hawakupewa muda wa kutosha ili kuondoa
mali zao kiustarabu na badala yake zoezi hilo kufanyika nyakati za
sikukuu ambapo asilimia kubwa ya wapangaji hao hawapo,hali iliyochangia
baadhi ya vibaka kutaka kuiba na kuambulia kipigo.
Kutokana na malalamiko hayo kuwa makubwa ikiwemo
wapangaji kusitishwa mikataba yao pamoja na kuondolewa katika nyumba
wakati wamelipa kodi hadi mwezi huu,ITV ilimtafuta mkurugenzi wa shirika
la nyumba la taifa bwana Nehemia Mchechu na kusema shirika hilo halina
nia mbaya ya kumwibia mtu hivyo waliolipa kodi zao wafike ofisini kwao
na watarejeshewa na kwamba walichokifanya ni jambo jema la kuwaondoa
watu katika nyumba hatarishi na pia wametii maagizo ya mahakama.
NA ITV