
Katika Mkoa wa Morogoro, kumekuwa na hali ya taharuki baada ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda, kudaiwa kupigwa risasi begani wakati polisi wakiwa katika harakati ya kuwatawanya wafuasi wa shekhe huyo na kumkamata Sheikh Ponda.
Wafuasi wake walionekana wakimsindikiza kwa maandamano kuelekea katika msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja akitokea katika viwanja vya Shule ya Kiwanja cha Ndege alikokuwa akihutubia kongamano.
Tukio hilo lilitokea jana saa 12.25 jioni katika Barabara ya Tumbaku baada ya kumalizika kwa mkutano wa kongamano lililoandaliwa na Jumuiya ya Wahadhiri wa Kiislamu Mkoa wa Morogoro.
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa sheikh Ponda alikuwa amepanda gari ndogo huku wafuasi wake wakimsindikiza na walipofika katika eneo la gereji mabomu ya machozi yalipigwa na polisi ambao waliokuwa kwenye magari ya polisi. Lengo kufyetua mabomu hayo ni kuwatawanya wafuasi wake na kumkamata Ponda.
Baada ya tukio hilo baadhi ya Waislam walimchukua sheikh Ponda kutoka katika gari lake na kumkimbizia katika gereji moja na kutoka wakiwa wamempakia katika pikipiki na kumkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.
Mlinzi mmoja wa lango namba moja alisema msururu wa pikipiki zaidi ya 50 ulifika, lakini pikipiki zote zilizuiliwa isipokuwa iliyokuwa imembeba sheikh Ponda na kwenda naye mpaka mapokezi.
Wakiwa katika eneo hilo magari kadhaa ya polisi yaliingia katika lango la hospitali hiyo na hivyo wafuasi wa sheikh Ponda wakalazimika kumbeba begani na kuruka naye kupitia lango namba mbili.
Taarifa zilizopatikana baadaye zinadaiwa kuwa Sheikh Ponda alipelekwa katika Hospitali ya Kiislamu ya Msamvu.
Lakini taarifa nyingine zinaeleza kwamba baadaye alitolewa katika hospitali ya Msamvu na kupelekwa kuhifadhiwa kusikojulikana.
Sheikh Ponda Akihutubia Mhadhara
Katika kongamano lililofanyika katika viwanja vya shule ya msingi kiwanja cha ndege, Shekhe ponda alisema kuwa matatizo ya kunyanyaswa na kuteswa kwa waislam yamekuwa yakichangiwa na serikali iliyoko madarakani na kuwataka waislam kuhakikisha kuwa katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015 wanachagua serikali mpya yenye kujali haki sawa.
Alisema kuwa wakazi wa Mtwara wameonesha mfano kwa waislam wa kudai haki yao ya msingi ya gesi iliyogunduliwa huko kwa kukataa gesi kutoka mpaka wakazi wa eneo hilo wanufaike kwanza hali ambayo alidai kuwa ilizua tafrani baada ya ya jeshi kupelekwa huko.
Kwa upande wake Amir wa wahadhiri wa dini ya kiislam wa mkoa wa dar es salaam, Shekhe Kondo Bungo mbali ya kuwakata waislam kuacha kung’ang’ani maisha magumu walionayo ambayo alidai yamesababisha na chama cha mapinduzi (CCM), aliwaponda viongozi wa dini hiyo ambao wamekuwa wakipokea na kula futari kutoka kwa watu wasiokuwa Waislam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile akizungumzia tukio hilo, amesema hadi kufikia jana usiku saa 2:00 hakuwa amepata taarifa zozote za kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na kwamba alikuwa amepata taarifa za awali kutoka kwa watu waliokuwa wakimpigia simu.
Chanzo: Nipashe, Mwananchi na Mitandao ya Kijamii.