Jaribio
la kuwatawanya wafanyakazi wa shirika la reli Tanzania na Zambia
(TAZARA) waliopo katika mgomo ulioingia siku ya nne kwa kutumia kikosi
cha askari wa kutuliza ghasia (FFU) limegonga mwamba baada ya askari hao
kufika eneo la tukio na kukaa kimya huku wakiwa na mabomu ya machozi na
muda mfupi kutoweka bila kufanya chochote.
Wafanyakazi
hao ambao walikuwa wamesimama nje ya jengo la TAZARA baada ya kuzuiliwa
kuingia ndani huku baadhi ya maeneo yakiwa yamezungushiwa ribon za
polisi kuashiria kuwa watu hawaruhusiwa kuingia eneo hilo, wafanyakazi
hao wamelalamikia kitendo hicho na kudai kuwa kimewadhalilisha na kudai
kuwa mgomo huo utaendelea hadi watakapolipwa haki zao.
Mgomo
huo umesababisha abiria waliokuwa wanasafiri kwa treni ya Tazara
kuendelea kukwama katika stesheni hiyo ambapo ITV imeshuhudia baadhi ya
abiria wakiwa kituoni hapo wakisubiri hatima ya safari zao huku baadhi
ya maofisa wakiendelea kukatisha tiketi ilihali wakijua uwezekano wa
kusafiri haupo.
Mmoja
wa viongozi wa wafanyakazi hao Bw Mussa Kalala amesema zoezi la mgomo
bado litaendelea na alipoulizwa hatua zilizochukuliwa na wahusika wa
tazara tangu waanze mgomo huo amesema hakuna kiongozi yeyote wa utawala
wameonana naye isipokuwa wamebandikiwa tu matangazo yanayodai kuwa
watalipwa mishahara yao agost 29 mwaka huu.
Kufuatia
sakata hilo itv imeutafuta uongozi wa Tazara ili kulitolea ufafanuzi
suala hilo ambapo afisa uhusiano wa Tazara Mkoa wa Tanzania Bi Regina
Tarimo mbali na kukiri kuwa madai yao ni ya kweli pia amesema tatizo
hilo kwa sasa linashughulikiwa na serikali zote mbili tanzania na
Zambia.
chanzo:itv