WAUMINI WAFUNGA KANISA NA KUMTIMUA MCHUNGAJI

KULITOKEA kizaazaa Jumapili asubuhi katika kanisa moja eneo la Mukurwe-ini, Kaunti ya Nyeri nchini Kenya baada ya kundi la waumini kumtimua pasta wao na kufunga kanisa kwa kufuli.
Baadhi ya waumini wa kanisa la Kanunga Baptist, Ichamara, walichukua hatua huyo wakimlaumu kasisi wao Bw Muriithi Mbote kwa kutowaletea maendeleo na kuwaongoza kwa njia isiyofaa.

Ibada ya asubuhi ilitatizika na ilibidi kundi la waumini wanaomuunga mkono Pasta Mbote kuomba nje ya lango la kanisa kabla ya polisi kuwasili ndiposa lango likafunguliwa.

Wapinzani wa pasta huyo walikuwa wameweka mabango katika lango la kanisa yakiwa na maandishi ya kumlaani huku tukio hilo likiwavutia wakazi waliokuwa wakielekea makanisa mengine kwa ibada.

Kundi linalompinga pasta huyo lilisema kanisa lao liko nyuma kimaendeleo kuliko makanisa mengine eneo hilo na ndiyo sababu walitaka pasta huyo ahamishwe.

Walimlaumu pasta huyo kwa kuzuia baadhi ya vijana kujiunga na kamati ya kanisa, wakisema alikuwa akiendesha shughuli za kanisa kwa njia isiyofuata kanuni za kanisa zinazowapatia waumini mamlaka ya kufanya maamuzi.

“Pasta Mbote amekuwa hapa kwa miaka 10 iliyopita sasa. Tunataka ahamishwe ili kanisa letu lipate nafasi ya kustawi,” akasema Bw Antony Muturi, muumini wa kanisa hilo. Hata hivyo, baada ya polisi kuingilia kati, makundi hayo mawili yaliandaa mkutano mfupi kwa amani na waliofunga lango wakafungua na kuruhusu ibada kuendelea.

Maandamano
Muumini mwingine Bw Samuel Kamiri, alisema walicholalamikia waumini hao hakikuhitaji maandamano, bali walipasa kuitisha mkutano na kamati ili kusuluhisha tofauti zao kwa amani.

“Tunaanika jambo hili kwa umma kwa njia isiyofaa. Tunafaa kuketi kama wangwana na kutafuta suluhisho,” akasema Bw Kamiri.

Akizungumza na wanahabari, Pasta Mbote alikanusha madai dhidi yake na kusema yuko tayari kuhama kanisa hilo ikiwa waumini hawakutaka aendelee kuhudumu.

“Sina uwezo wa kulazimisha jinsi kanisa linapasa kusimamiwa. Ni kamati ya kanisa iliyo na mamlaka ya kufanya hivyo,” akasema Pasta Mbote.

Alisema kamwe hakuwa na habari kuhusu mambo aliyolaumiwa na wapinzani wake kuhusu na kuongeza kwamba amekuwa akihusisha waumini katika maamuzi ya jinsi ya kusimamia kanisa hilo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo