Wananchi wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kuhakikisha wanaacha mara moja utaratibu wa kupanda miti kwenye mashamba ya kulimia kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha kupunguza kasi ya uzalishaji wa mazao ya kulimia
Kauli hiyo imetolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh. Jison Mbalizi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya serikali za mitaa yaliyofanyika kiwilaya katika kata ya Kipagalo wilayani Makete
Mh Mbalizi amesema ipo hatari ya wilaya ya Makete kukumbwa na baa la njaa siku za usoni kutokana na mashamba yaliyotengwa kwa ajili ya mazao ya chakula kupandwa miti hivyo uzalishaji lazima upungue
"Jamani wananchi huu ni muda wa kubadilika, kama mashamba yote yakijaa miti tutapata wapi mashamba ya kulimia mazao yetu ya kula? hapa tunajitafutia njaa wenyewe ndugu zangu hebu tubadilike maana tunaona kama masihara lakini ipo siku mtaikumbuka kauli hii" alisema Mbalizi
Pamoja na mambo mengine Mbalizi amewataka watu kujijengea utaratibu wa kupima magonjwa mbalimbali kwa hiari hasa virusi vya UKIMWI kwani kutasaidia wao kufahamu afya zao na kuchukua tahadhari kwa kuwa wanafahamu hali zao
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mahulu Bw. Erasto Mwalukisa ameitaka serikali kuhakikisha inawahisha fedha za miradi ya maendeleo vijijini mapema ili miradi ikamilike kwa wakati, ujenzi wa nyumba za watumishi pamoja na wananchi kujengewa uwezo wa kuzifahamu sheria mbalimbali za nchi
katika maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila Julai mosi Mgeni rasmi alipata wasaaa wakutembelea mabanda mbalimbali yaliyokuwa eneo la maadhimisho na kupewa maelezo namna idara mbalimbali za halmashauri zinavyofanya kazi ikiwemo idara ya afya, kilimo, utawala pamoja na elimu
picha za tukio hilo zitakujia baadaye