Rais wa Amerika Barack Obama na Mkewe Michelle wapungia watu mikono
kabla ya kuingia Air Force One na kuondoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege
wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Tanzania Julai 2, 2013. Picha/AFP
Na REGINALD MIRUKO Na BONIFACE MEENA / MWANANCHI
RAIS wa Amerika Barack Obama ameondoka
nchini muda huu kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere
huku maelfu ya wananchi wa Tanzania wakijitokeza barabarani kumuaga.
Rais Obama
alikuwa nchini humo katika ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo ametaja
vipaumbele vinne vya Marekani kwa Tanzania, ambavyo vinajumuisha miradi
mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji na programu za
kielimu kwa vijana kwa lengo la kuongeza ajira
Jijini Dar es
salaam Barabara za Ally Hassan Mwinyi, Mandela, Sam Nujoma na ile ya
Morogoro zilifungwa kwa muda kuanzia majira ya saa tatu asubuhi huku
maelfu ya wananchi wakitanda barabarani kwa lengo la kumuaga rais huyo.
Mara baada ya
kufika katika uwanja wa Ndege Rais Obama na Mkewe walitumia muda
mfupi kuagana na mwenyeji wao Rais Kikwete na mkewe ikiwa ni pamoja na
kuwaaga mamia ya viongozi waliofika uwanjani hapo.
Wakati wa ziara hiyo yake,
Obama alitaja vipaumbele vinne vya Marekani kwa Tanzania, ambavyo
vinajumuisha miradi mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji
na programu za vijana kwa lengo la kuongeza ajira.
Kiongozi huyo
aliwasili Dar es Salaam Jumatatu mchana ikiwa ni nchi ya mwisho katika
ziara yake barani Afrika ikitanguliwa na Senegal na Afrika Kusini.
Akizungumza
na waandishi wa habari pamoja na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, Rais Obama
alisema aliainisha mambo hayo wakati alipozungumza na mwenyeji wake
huyo.
Alisema
katika mazungumzo hayo, waligusia mradi wa mkubwa wa umeme uitwao Power
Afrika wenye lengo la kuongeza kiwango cha umeme kinachozalishwa nchini
na barani Afrika ili kupata umeme nafuu na wa uhakika utakaochagiza
kuongeza uzalishaji na kukuza ajira.
Nchi nyingine za Afrika ambazo zitanufaika na mpango huo ni Kenya, Ghana, Liberia, Nigeria na Ethiopia.
Rais Obama
alisema pia wamezungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo, ukuzaji wa
demokrasia na utawala bora.
Alimzungumzia pia mchezaji nyota wa mpira wa
kikapu wa Tanzania, Hashimu Thabeet anayecheza katika Ligi Kuu ya
Marekani (NBA), akiwa na timu ya Oklahoma Thunder ya Marekani, akisema
hawakuzungumzia suala lake na kuahidi kufanya hivyo siku nyingine.
Akijibu swali
iwapo anaridhishwa na misaada ambayo nchi yake inatoa kwa Tanzania,
Rais Obama alisema anafarijika kwa matunda yanayopatikana katika
mapambano dhidi ya malaria, barabara mpya zinazojengwa na katika maeneo
mbalimbali ya nchi.
“Hatutoi
dawa, bali tunajenga miundombinu ya afya, hatutoi chakula, bali
kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula pia tunasisitiza kubadilishwa
kwa sheria mbalimbali ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kuleta mitaji
yao kwa wingi zaidi, lakini jambo la muhimu ni kuijenga Afrika,”
alisema.
Kuhusu sekta
ya utalii, Rais Obama alisema watatangaza vivutio vya Tanzania, lakini
kwa kuwa ameambiwa ujangili ni tatizo, Serikali yake itaisaidia Tanzania
kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tutatangaza
utalii, nimeelezwa ujangili ni tatizo hivyo Marekani itasaidia kupambana
na changamoto hiyo na tutaongeza fedha kuhakikisha hali hiyo
inatokomea,” alisema.
Akichangia
hoja ya misaada ya Marekani, Rais Kikwete alisema Mradi wa Maendeleo ya
Changamoto za Milenia (MCC), umekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania.
Alisema
kupitia MCC, Tanzania imepata msaada wa kujengewa barabara katika maeneo
ya vijijini na yale yanayozalisha chakula kwa wingi.
Aliyataja
baadhi ya maeneo ambayo yamenufaika kwa barabara hizo kuwa ni Namtumbo,
Songea, Mbinga, Tunduma, Horohoro, Tanga na baadhi katika Kisiwa cha
Pemba.
Alisema
Tanzania pia imenufaika kwa mradi wa maji jijini Dar es Salaam ambao
ujenzi wake unaendelea na umeme kwa ajili ya maeneo ya vijijini ambao
pia unafadhiliwa na Marekani katika mikoa 10 ya Tanzania.
“Kusema kweli
Marekani imefanya makubwa, nikisema inatosha, Mheshimiwa Rais
hatasikiliza maombi yangu mengine,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete
alisema kutokana na misaada ya Marekani, maambukizo ya Ukimwi
yamepungua, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua na wale
wanaozaliwa na wakiwa na VVU wamepungua kwa kiwango kikubwa.
Alisema pia
Watanzania wamenufaika na msaada wa vitabu milioni mbili vya sayansi.
Alitumia fursa hiyo kuomba idadi nyingine kama hiyo.
“Nimemwambia
tunaomba vitabu vingine milioni mbili na yeye akasema niongee na watu
wake, lakini nilipowatazama nikaona nyuso zao zinakubaliana na Rais
wao,” alisema Kikwete.
Katika hatua
nyingine, Rais Kikwete aliulizwa kuhusu kesi ya Mtanzania aliyeshtakiwa
Marekani kwa kumtumikisha binti wa Kitanzania na kushindwa kulipa faini
na kusema analifahamu suala hilo, lakini limemalizika kwa wahusika
kulipwa.
Alisema binti
aliyelalamika alichukuliwa na dada yake kwenda kusomeshwa Marekani,
lakini alipofika akatumikishwa kwa kazi za ndani aliwashtaki dada yake
na shemeji yake na mahakama ikawatoza faini ya Dola milioni moja za
Marekani.
Hata hivyo,
alisema haikuwa rahisi kwa wadaiwa kulipa faini hiyo kutokana uwezo wao
mdogo, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, hivyo waliomba faini
ipunguzwe na ilipopunguzwa ikalipwa na suala hilo likamalizika.
Aifagilia Tanzania
Akiizungumzia
Tanzania, Obama alisema, “Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Tanzania,
mzee wangu alikuwa Afrika Mashariki na wakati fulani aliishi Tanzania,
mke wangu na watoto wangu wamefurahi kufika hapa.
Alisema
alipoingia madarakani Rais wa kwanza kutoka Afrika kukutana naye alikuwa
ni Rais Kikwete kwa kuwa Tanzania inaheshimu utawala wa kidemokrasia.
Obama alisema
Tanzania imefanya kazi nzuri pamoja na Zanzibar kwa kufanikisha suala
la Katiba Mpya kwa ajili ya Tanzania ijayo kwani hiyo ndiyo demokrasia.
Pia
aliipongeza Tanzania kuhusu hatua yake katika kulinda amani katika nchi
za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Sudan hasa eneo la Darfur.
Alisema DRC inaathiriwa na machafuko kutokana na kuwa na maliasili
nyingi na kusema Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila na watu wake
wanahitaji kufanya kazi kubwa kuhakikisha amani inakuwapo.