PADRI AFUNGA KANISA KWA KUTUMIA JENEZA

 
PADRI wa kanisa Katoliki alizua sokomoko alipofunga kanisa kwa jeneza na kuzuia misa kufanyika.
Kisa hicho cha kushangaza kilitokea katika kanisa la Taru, Dayosisi Kuu ya Mombasa na kupelekea Padri Thomas Apil kukabiliwa vikali na waumini

Ilibidi polisi kutoka kituo cha Taru kuitwa kumuokoa padri huyo asiumizwe na waumini wake.

Padri Api amekuwa na mgogoro katika parishi ya Taru tangu ahamishiwe huko mwaka mmoja uliopita kuchukua mahali pa Padri Henry Katana ambaye alipata uhamisho wa ghafla.
Afisa Mkuu wa polisi wilayani Kinango Bw Silas Ringera alisema ilibidi awatume maafisa wake kumuokoa padre huyo kutokana na fujo baada ya kuleta jeneza kanisani na kuzuia waumini kuingia kwa misa.

Jumapili iliyotangulia, waumini waliokuwa na hasira walifunga nyumba ya padri huyo na kanisa na kumuamuru aondoke. Hata hivyo, walishangaa walipomuona amebeba jeneza hapo Jumamosi jioni ambalo alilitumia kuzuia waumini kuingia kanisani

“Padre huyo aliandamana na wanafunzi wawili wa seminari ambao aliingia nao kanisani na kuendesha ibada baada ya kufunga kanisa kwa jeneza,” alisema mwumini. Padri Apil alivaa nguo nyekundu siku hiyo.

Akiongea baada ya kisa hicho, padri huyo alisema alipotumwa kuhudumu mahala hapo hakupokelewa vyema. “Najua ni kwa sababu mimi sitoki katika jamii ya Wamijikenda kama alivyokuwa Padri Henry Katana,” alisema.

Lakini waumini walipuuzilia mbali madai hayo wakisema padri huyo ndiye aliyejiletea shida.

Walisema mapadri wengi wakiwemo Wazungu na kutoka makabila mbalimbali washahudumu hapo pasipo matatizo.
Walimlaumu padri huyo kwa tabia isiyoridhisha kama vile kuleta wanawake nyumbani kwake na kuvunjilia mbali mashirika yote ya kanisa hilo.

Mwenyekiti wa kamati ya parokia hiyo Bw Raphael Galuka majuzi aliongoza ujumbe kumuona Askofu Lele na kumtaka amhamishe padri huyo. Hata hivyo, askofu huyo hakuchukua hatua yoyote.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo