Rais wa Amerika Barack Obama na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete
wakisalimia watu waliofika kumlaki Obama baada ya kuwasili Tanzania
Julai 1, 2013. Picha/AFP
Maelfu ya
wakazi wa Dar es Salaam, walijitokeza kwa wingi Jumatatu kumlaki Rais wa
Marekani, Barack Obama aliyewasili nchini kwa ziara ya siku mbili
inayohitimishwa leo huku wakilalamikia kutomwona.
Kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, msafara wake ulipitia Barabara
za Nyerere, Nkrumah, Samora, Magogoni hadi Ikulu.
Ukonga Majumba Sita
Wakazi wa
maeneo ya Gongo la Mboto, Ukonga, Kitunda, na Tabata walifurika eneo la
Majumba Sita kwa ajili ya kumwona, lakini hali ilikuwa tofauti.
Magari
yalizuiwa kuanzia Njia panda ya Segerea na hayakuruhusiwa kusogea karibu
na barabara inayotoka uwanja wa ndege. “Mimi nimefika hapa kwa ajili ya
kumwona, sikumwona jamani yaani nimepigwa na jua bure,” alilalamika
dada mmoja akiwa na wenzake huku ameshikilia kandambili mkononi.
Naye Mkazi wa
Tabata Mawezi, aliyejitambulisha kwa jina la Jana Kamanzi alilalamikia
mwendo kasi wa magari hayo na kushindwa kumuona kiongozi huyo.
Kipawa/Jeti Lumo
Maeneo hayo walijitokeza watu wengi huku wengine wakiwa na mikeka ya kukalia tayari kumlaki kiongozi huyo.
Gazeti hili lilishuhudia umati huo kwa wakazi kutoka maeneo ya Jeti, Kipawa, Karakata waliofika kumlaki Rais huyo wa Marekani.
Baadhi ya
mama lishe walitumia nafasi hiyo kuuza chakula kwenye ndoo za plastiki
kwa kificho, huku wafanyabiashara ya maji na wao wakitumia nafasi hiyo
kupandisha bei ya maji huku wakiuza kwa kificho.
Vingunguti
Katika maeneo
ya Vingunguti, umati ulifurika pande zote mbili za barabara kwa wakazi
wa Vingunguti na Kijiwe Samli wakiwamo wafanyakazi ambao ofisi zao ziko
karibu na Barabara ya Nyerere.
Maafisa
Usalama waliokuwa wamejichanganya na wananchi, walimkamata mama mmoja
aliyekuwa akijaribu kuvuka barabara kabla ya msafara wa Rais Jakaya
Kikwete kupita wakati akienda kumpokea mwenyeji wake, Rais Obama.
Kwa kuwa kila
mmoja alikuwa akimwangalia, wakati anajiandaa kukatisha barabara na
msafara unakuja, walimkimbilia na kumdaka na kisha kuondoka naye. Hata
hivyo haikuweza kufahamika mama huyo alikuwa na lengo gani.
Magari yalizuiwa kutoka Vingunguti na hata yale yanayotokea Kijiwe Samli, barabara zake zinaingia Barabara ya Nyerere.
Baadhi ya wakazi hao walisikika wakilalamika kutomwona Rais Obama kwani walitarajia angekuwa kwenye gari la wazi waweze kumuona.
Wakazi
wengine walilalamikia hali hiyo, mbali na kutotarajia umati na kushindwa
kumwona, walijua kuwa atakuwa kwenye gari la wazi ambalo wangeweza
kumuona.
Makutano ya Mandela na Nyerere (Tazara)
Wananchi walivamia msafara wa Rais Obama katika eneo la Tazara na kusababisha msafara huo kupunguza mwendo.
Kitendo hicho
kilitokea wakati Rais huyo na msafara wake uliokuwa na zaidi ya magari
15 ukitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ukienda Ikulu.
Msafara wa
Rais Obama haukuwa katika mwendo wa kasi na ulipokaribia makutano ya
barabara hizo maeneo ya Tazara, wananchi walivuka kutoka upande wa pili
kushuhudia msafara huo kwa ukaribu zaidi.
Kitendo hicho
cha wananchi kuvamia msafara huo kwa ghafla kiliwachanganya askari
polisi waliokuwa wachache, hivyo kusababisha msafara huo kupunguza
mwendo.
Awali askari
Polisi waliimarisha ulinzi na kuwazuia watu kuvuka barabara kutokana na
magari kupita kwa kasi eneo hilo na wananchi walitiii amari hiyo.
Njia Panda ya Veta
Katika maeneo
yanayounganisha Barabara ya Nyerere na Chang’ombe, polisi walifanya
kazi ya ziada kuzuia mamia ya watu waliofika kumlaki .
Mamia ya watu
hao kutoka Temeke, Chang’ombe, Tandika, Ilala walifurika katika eneo
hilo kutaka kumuona kiongozi huyo, lakini hata hivyo wengi walisikika
pia wakilalamikia kutomwona.
Kamata
Wakazi wa maeneo ya Kariakoo, Gerezani, Ilala walifurika kuanzia njia panda ya Shauri Moyo huku wakiwa katika hali ya utulivu.
Polisi walikuwa na kazi ya kuzuia wakazi hao waliokuwa wanavuka barabara kabla na baada ya misafara kupita.
Mtaa wa Nkrumah
Hali ilikuwa
tete katika Mtaa wa Nkrumah ambako ulipita msafara wa Obama wakati
akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.Msafara wa Rais
Obama ulipita katika Mtaa wa Nkrumah kwa ajili ya kuingia Mtaa wa Samora
kuelekea Ikulu.
Maduka na
ofisi kadhaa zilizoko maeneo ya Nkrumah, Kidongo Chekundu na Mnazi Mmoja
yalifungwa kutokana na watu kuwa na hamu ya kuuona msafara wa Obama.
Watu walikuwa wengi pande zote za barabara na msafara wa Obama ulipofika
kwenye eneo hilo, watu walimshangilia kwa nguvu
Hata hivyo,
watu wengi walisikitishwa na kitendo cha kutomwona Obama kwani wengi
walitegemea kuwa watapanda gari lenye vioo ambavyo wangeweza kumwona kwa
urahisi wakati akipita katika eneo hilo la Nkrumah.
NA MWANANCHI, DAR ES SALAAM